Mkurugenzi wa kampuni ya uajiri amefikishwa mahakamani jijini Nairobi akikabiliwa na mashtaka ya kuwalaghai Wakenya wanaotafuta ajira nchini Uingereza kiasi cha Sh20 milioni.

Alphonse Kioko Kivindu, mwenye umri wa miaka 58, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Amble Beginning Consult Limited, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Milimani Geoffrey Onsarigo, ambako alikanusha mashtaka 12 dhidi yake.

Kivindu anakabiliwa na mashtaka mbalimbali, yakiwemo ya kula njama ya kutenda uhalifu, kupata fedha kwa njia ya udanganyifu na kupokea mapato yanayotokana na uhalifu.

Mahakama ilielezwa kuwa kati ya Januari 2023 na Februari 2024, mshtakiwa alidaiwa kupokea Sh18.5 milioni kutoka kwa Joyce Wambui Njihia kwa madai ya kumhakikishia nafasi ya kazi nchini Uingereza.

Katika tukio jingine, Kivindu anadaiwa kupokea Sh200,000 kutoka kwa Frasiah Wambui Kinyua mnamo Aprili 13, 2023.

Pia anadaiwa kuchukua Sh500,000 kutoka kwa Mary Waithira Mburu kati ya Aprili 11 na 18 mwaka huo huo, huku Agnes Wanjiku Mandu akidaiwa kumpa Sh850,000 kati ya Juni na Novemba 2023.

Fedha hizo zilitolewa kwa matumaini ya kupata nafasi za ajira nchini Uingereza, lakini nafasi hizo hazikupatikana kama ilivyoahidiwa.

Upande wa mashtaka ulieleza kuwa fedha zilizopokelewa na mshtakiwa zinadaiwa kuwa mapato yaliyotokana na uhalifu, na hivyo kumfungulia mashtaka chini ya Sheria ya Mapato ya Uhalifu na Kupambana na Utakatishaji Fedha.

Mashtaka ya kupata fedha kwa njia ya udanganyifu yanatokana na Kifungu cha 313 cha Kanuni ya Adhabu.

Kivindu alikamatwa Novemba 3, 2026, na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI),Machakos.

Wakili wake aliomba mahakama kumpa masharti nafuu ya dhamana, akisema mteja wake hana hatari ya kutoroka na yuko tayari kuhudhuria vikao vyote vya mahakama.

Hakimu Onsarigo aliamuru mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana ya Sh5 milioni au fedha taslimu Sh1 milioni, pamoja na watu wawili wa kumtambulisha.

Kesi hiyo itatajwa tena kwa ajili ya maelekezo ya maandalizi ya kusikilizwa, huku upande wa mashtaka ukitarajiwa kuwasilisha taarifa za mashahidi na vielelezo kwa upande wa utetezi.