Jaji Mkuu Martha Koome ameonya watu wanaofadhili makundi ya wahuni nchini kuwa hawataepuka mkono wa sheria, akisisitiza kuwa wanaochochea vurugu lazima wawajibishwe pamoja na wanaotekeleza uhalifu huo.

Koome alitoa kauli hiyo alipofungua rasmi Mahakama ya Maara katika Kaunti ya Tharaka Nithi, akitetea matamshi yake ya awali kuhusu kufunguliwa mashtaka kwa wafadhili wa makundi ya wahuni chini ya sheria zinazokabili makosa makubwa ya jinai.

Jaji Mkuu alisema ni muhimu kuhakikisha wanaofadhili na kuratibu vitendo vya kihalifu wanakabiliwa na sheria badala ya kuwaacha vijana wanaotumiwa kutekeleza vurugu pekee wakikamatwa huku wanaowatuma wakiendelea kuwa huru.

Kauli yake iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Muthomi Njuki, ambaye alisema vita dhidi ya makundi ya wahuni haviwezi kufanikiwa iwapo hatua zitachukuliwa dhidi ya vijana wanaotekeleza vitendo hivyo bila kuwafikia wafadhili wao.

Njuki alisisitiza kuwa wafadhili na wafadhili wakuu wa makundi hayo wanapaswa kufikishwa mahakamani ili kukomesha tabia ya kutumia vijana kufanya uhalifu huku wanaowafadhili wakijikinga dhidi ya sheria.

Katika kikao hicho, Koome pia alionya maafisa wa usalama na wachunguzi wanaozuia haki kutendeka katika kesi za unyanyasaji wa kingono na ubakaji wa watoto kwa kuruhusu mazungumzo ya nje ya mahakama yanayoweza kuathiri mwenendo wa kesi.

Alisema maafisa watakaopatikana wakitatiza mchakato wa haki katika kesi hizo wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kukiuka misingi ya utoaji haki.

Ziara hiyo pia iliashiria kufunguliwa rasmi kwa Mahakama ya Maara, iliyojengwa kupitia ushirikiano wa Mbunge wa eneo hilo Kareke Mbiuki na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

Mahakama hiyo imekuwa ya 151 ya mahakimu nchini, huku Koome akiahidi kuongeza idadi ya mahakama hadi 200 kabla ya kumalizika kwa muhula wake.

Kufunguliwa kwa mahakama hiyo kunatarajiwa kupunguza msongamano katika Mahakama ya Chuka, ambapo jumla ya kesi 269 zitahamishiwa Maara, ikiwemo takriban kesi 100 zinazohusu migogoro ya ardhi.

Mahakama hiyo inatarajiwa kuanza rasmi shughuli zake Januari 4, 2027, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wakazi wa Maara na maeneo jirani.