Rais William Ruto anatarajiwa kuzindua ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta cha East Africa Refinery mjini Lamu, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya maendeleo katika kaunti sita za Pwani.
Mradi huo unaokadiriwa kugharimu takriban dola bilioni 16, sawa na zaidi ya Sh2 trilioni, unatarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano unaohusisha serikali ya Kenya na mfanyabiashara wa Nigeria Aliko Dangote.
Rais Ruto amesema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kusafisha hadi mapipa 700,000 ya mafuta kwa siku. Uzinduzi rasmi wa ujenzi umepangwa kufanyika Septemba 30, 2026.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kusafisha mafuta ghafi, yakiwemo yanayotarajiwa kuzalishwa Lokichar, Turkana, na kusambaza bidhaa za petroli katika masoko ya Afrika Mashariki na Kati.
Serikali inasema mradi huo utasaidia kuimarisha usalama wa nishati nchini, kupunguza utegemezi wa mafuta yaliyosafishwa kutoka nje na kufungua fursa za kiuchumi.
Kabla ya uzinduzi huo, Rais Ruto alikutana na Dangote pamoja na Rais na Afisa Mkuu Mtendaji wa Africa Finance Corporation (AFC), Samaila Zubairu, mjini New York kujadili ufadhili na maandalizi ya mradi huo.
Ruto pia alitembelea kiwanda cha Dangote Petroleum Refinery mjini Lagos, Nigeria, Ijumaa kabla ya kurejea Kenya.
Mbali na mradi wa Lamu, Rais Ruto anatarajiwa kuanza ziara ya maendeleo katika eneo la Pwani Jumamosi, akitembelea kaunti za Taita-Taveta, Kwale, Kilifi, Mombasa, Tana River na Lamu.
Katika ziara hiyo, Rais anatarajiwa kutoa karibu hati miliki 200,000 za ardhi kwa wakazi wa Pwani ikiwa ni sehemu ya mpango wa serikali wa kushughulikia changamoto za muda mrefu za umiliki wa ardhi katika eneo hilo.
Taita-Taveta inatarajiwa kupata hati miliki 31,318 zitakazotolewa kwa wakazi wa maeneo ya Mwatate na Voi.
Katika Kaunti ya Kwale, hati miliki 94,175 zinatarajiwa kutolewa kwa wakazi wa Lunga Lunga, Msambweni na Kinango, huku Kilifi ikipata hati 36,826 kwa wakazi wa Kaloleni, Rabai, Ganze, Kilifi Kusini na Malindi.
Mombasa inatarajiwa kupata hati miliki 4,360, huku jumla ya hati 22,770 zikitarajiwa kutolewa kwa wananchi wa Lamu na Tana River.
Serikali inasema utoaji wa hati hizo ni sehemu ya mpango mpana wa kutoa hati miliki 500,000 katika eneo la Pwani ili kutatua migogoro ya kihistoria ya ardhi na kuwapa wananchi usalama zaidi wa umiliki wa mali zao.
Katika ziara hiyo, Rais pia anatarajiwa kuzindua miradi iliyokamilika, kukagua inayoendelea na kuanzisha miradi mipya ya maendeleo katika kaunti hizo sita.




