Uchimbaji madini ni shughuli inayowapa watu wengi nafasi ya kujipatia riziki, wakiwemo wale ambao hawakupata fursa ya kuendelea na masomo.

Kupitia kazi za kuchimba, kubeba mawe, kuchambua udongo na kuuza madini, baadhi ya wakazi huweza kujikimu kimaisha na kusaidia familia zao.

Hata hivyo, shughuli hizo zinapogusa haki za umiliki wa ardhi na maslahi ya jamii, masuala ya kisheria huwa muhimu katika kuhakikisha kuwa wananchi hawapotezi haki zao.

Hali hiyo imejitokeza katika eneo la Ramula, Kaunti ya Siaya, baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi kutoa amri zinazozuia kampuni ya Shanta Gold kutekeleza shughuli za uchimbaji na utafutaji wa madini katika baadhi ya maeneo ya Ramula, Munungu na Uranga bila idhini ya wazi ya wamiliki halali wa ardhi.

Katika uamuzi wake, mahakama ilizuia kampuni hiyo kuingia katika ardhi za kibinafsi, kufanya utafiti au uchimbaji wa majaribio, kukata mimea, kuchimba mashimo au kutekeleza shughuli nyingine zozote kwenye vipande vya ardhi ambavyo wamiliki wake hawajatoa idhini inayohitajika kisheria.

Mahakama ilisisitiza kuwa haki ya kumiliki mali inalindwa na Katiba na kwamba kampuni zinazotafuta kufanya shughuli za uchimbaji lazima zifuate masharti yaliyowekwa na sheria.

Ilieleza kuwa Kifungu cha 37(1) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2016 kinahitaji idhini ya wazi ya wamiliki waliosajiliwa kabla ya haki za utafutaji na uchimbaji kutolewa kwa ardhi ya kibinafsi.

Pia, mahakama ilikosoa namna mamlaka husika ya serikali ilivyoshughulikia leseni ya utafutaji madini PL 2019-0222, iliyotolewa Agosti 1, 2019, ikisema mchakato huo haukuzingatia kikamilifu masharti ya Kifungu cha 34 cha Sheria ya Madini.

Katika hatua nyingine, mahakama ilielekeza kuwa leseni ya uchimbaji inayohusiana na mradi wa Ramula, kupitia ombi nambari 0200, isitolewe kwa maeneo yaliyoathiriwa hadi mamlaka husika zithibitishe kwa nyaraka kuwa wamiliki wote wa ardhi zinazohusika wametoa idhini yao.

Bodi ya Haki za Madini pia imeagizwa kuzingatia vibali vinavyohitajika kisheria, vikiwemo vile kutoka kwa Serikali ya Kaunti ya Siaya pale vinapohitajika.

Mahakama iliamuru kuwa pingamizi zilizowasilishwa kufuatia notisi iliyochapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali mnamo Agosti 1, 2025, pamoja na pingamizi za awali za waombaji kesi, zisikilizwe upya kabla ya uamuzi wowote kuhusu ombi la leseni kufanywa.

Aidha, mamlaka husika zimezuiwa kuchukua hatua za kuwahamisha au kuwafurusha wakazi wa Ramula, Munungu na Uranga kinyume na masharti ya Kifungu cha 153 cha Sheria ya Madini.

Mahakama pia ilielekeza kuwa leseni isitolewe hadi mfumo wa makubaliano kuhusu ugavi wa manufaa yatakayotokana na mradi huo uwekwe kwa mujibu wa Katiba na sheria zinazohusika.

Kuhusu upatikanaji wa taarifa, mahakama ilibainisha kuwa wakazi walikuwa wamewasilisha malalamishi kuhusu juhudi zao za kupata maelezo kuhusu mradi na uzingatiaji wa sheria za madini na mazingira.

Ingawa taarifa fulani zilikuwa zimetolewa na mamlaka za serikali kupitia njia rasmi, mahakama ilisema kutokujibu maombi ya taarifa yaliyotumwa kwa kampuni hiyo hakukuwa jambo la kuridhisha.

Kesi hiyo, nambari 003 ya mwaka 2025, ilifanikiwa kwa sehemu, huku amri za mahakama zikilenga kulinda haki za wamiliki wa ardhi na kuhakikisha kuwa shughuli zozote za uchimbaji katika eneo hilo zinafuata sheria.