Wafanyabiashara katika ufuo wa Dunga Beach, Kaunti ya Kisumu, wanakadiria hasara baada ya mvua kubwa iliyoandamana na upepo mkali kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na kuwaacha watu wanne wakiuguza majeraha.
Dhoruba hiyo iliyoshuhudiwa Jumapili jioni ilisababisha kubomoka kwa hoteli nne, huku miundo mingi ya biashara ya muda ikisombwa na upepo, na kuwaacha wafanyabiashara wakijaribu kuokoa mali zilizobaki.
Baadhi ya wafanyabiashara wameanza kukarabati na kuimarisha miundo yao wakihofia huenda mvua nyingine kubwa ikasababisha uharibifu zaidi, huku wengine wakibaki wakikodolea macho mabaki ya biashara zao yaliyotawanyika ardhini.
Mwenyekiti wa soko la samaki la Dunga, Millicent Atieno Ogada, amesema watu kadhaa walijeruhiwa baada ya vitu mbalimbali kuanguka kutokana na nguvu ya upepo na mvua iliyonyesha.
Ogada amesema eneo la kivuli walichokuwa wakitumia wafanyabiashara wa samaki pia liliharibiwa, hali iliyozidisha changamoto kwa wafanyabiashara ambao tayari wanakabiliwa na hasara kutokana na kusitishwa kwa shughuli zao za kawaida.
Amesema wafanyabiashara bado wana hofu kutokana na utabiri wa hali ya hewa unaoonyesha kuwa mvua kubwa zinaweza kuendelea kunyesha katika eneo hilo.
Ametoa wito kwa viongozi wa eneo hilo na mamlaka za usimamizi wa majanga kuingilia kati kwa kutoa msaada kwa waathiriwa ili waweze kurejelea shughuli zao za kiuchumi.
Francisca Odhiambo, ambaye pia ni mfanyabiashara katika ufuo huo, amesema tukio hilo liliwaacha wafanyabiashara wengi katika hali ya mshtuko, huku baadhi yao wakishindwa kurejelea shughuli zao kutokana na hofu ya kukumbwa tena na dhoruba kama hiyo.
Wakati wafanyabiashara wa Dunga wakihesabu hasara, wakazi wa kijiji cha Em'machika katika Kaunti ya Vihiga pia wameathirika baada ya upepo mkali kuharibu nyumba tatu na kubomoa mimea mashambani.
Uharibifu huo unaongeza wasiwasi kuhusu usalama wa wananchi na athari za mvua kwa shughuli za kilimo na biashara, ambazo ni tegemeo la familia nyingi katika maeneo hayo.
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini (KMD) ilikuwa imetoa tahadhari kuhusu uwezekano wa mvua kubwa, upepo mkali na radi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Bonde la Ziwa Victoria na Pwani.
Utabiri wa hivi karibuni pia unaonyesha uwezekano wa kuendelea kwa mvua kubwa, hali inayowafanya waathiriwa kusubiri msaada wa dharura kutoka kwa mamlaka husika ili kurejesha maisha yao na kuzuia hasara zaidi.









