Operesheni ya kimataifa iliyolenga kuvunja mitandao ya uhalifu inayohusika na usafirishaji haramu wa wahamiaji kupitia Bahari ya Mediterania na njia ya Atlantiki katika Afrika Magharibi imewawezesha maafisa wa usalama kuwakamata washukiwa 262 na kufungua uchunguzi mpya 434.

Operesheni hiyo iliyopewa jina la Communis Maris, iliyofanyika kati ya Oktoba 5 na 8, 2026, pia ilibaini watu 109 wanaoshukiwa kuwa wahanga wa biashara haramu ya binadamu na kugundua wahamiaji 1,715 waliokuwa wameingia au kusafiri kinyume cha sheria.

Kati ya washukiwa waliokamatwa, 221 wanakabiliwa na tuhuma za kusafirisha wahamiaji kinyume cha sheria, 16 wanashukiwa kuhusika na biashara haramu ya binadamu, huku wengine 25 wakikabiliwa na makosa mbalimbali yakiwemo kutengeneza na kutumia nyaraka bandia.

Operesheni hiyo iliwahusisha maafisa wa usalama na udhibiti wa mipaka kutoka nchi 16 za Afrika Kaskazini na Magharibi, Ulaya Kusini na Mashariki ya Kati.

Iliendeshwa na Shirika la Kimataifa la Polisi (INTERPOL), kwa ushirikiano na Europol, Frontex, AFRIPOL, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).

Jumla ya maafisa 7,660 walishiriki katika operesheni hiyo, wakikagua zaidi ya watu 378,000 na kufanya ukaguzi katika maeneo yanayotumiwa na mitandao ya wasafirishaji haramu wa binadamu.

Katika tukio moja kusini mwa Morocco, mamlaka zilikamata boti iliyokuwa imebeba watu 70 waliokuwa wakijaribu kuhamia nchi nyingine, wakiwemo watoto 30. Abiria hao walikuwa wamekaa baharini kwa siku sita.

Katika tukio jingine, mamlaka ya Mauritania ilikamata boti ya mbao iliyokuwa imebeba watu 80, wakiwemo watoto wawili, baada ya kuarifiwa na maafisa wa Senegal. Washukiwa watatu wanaodaiwa kuandaa safari hiyo walikamatwa.

Nchini Libya, mamlaka ziliwaokoa watu 34 wanaoshukiwa kuwa wahanga wa biashara haramu ya binadamu na kuwakamata watu watatu wanaodaiwa kuhusika na mtandao wa uhalifu.

Aidha, mamlaka nchini Algeria ziliwakamata washukiwa sita, huku nchini Syria washukiwa saba, akiwemo anayedaiwa kuwa kiongozi wa mtandao huo, wakikamatwa pamoja na wahamiaji 22.

Operesheni hiyo pia ililenga viwanja vya ndege, ambapo washukiwa walikamatwa Cyprus na Ugiriki kwa kujaribu kutumia nyaraka bandia za kusafiria. Nchini Ufaransa, watu sita walikamatwa kwa tuhuma za utakatishaji fedha na kuwezesha uhamiaji haramu.

Mkurugenzi wa INTERPOL anayeshughulikia doria, David Caunter, amesema njia ya Bahari ya Mediterania ni miongoni mwa hatari zaidi za uhamiaji duniani, huku maelfu ya watu wakipoteza maisha kila mwaka.

Amesema wahamiaji hutumiwa vibaya na mitandao hiyo kupitia ulaghai, unyang'anyi na biashara haramu ya binadamu, huku wakisafirishwa kwa boti zisizo salama na zilizosheheni abiria.

INTERPOL inatarajia uchunguzi mpya ulioanzishwa kutoa taarifa zaidi zitakazowezesha kukamatwa kwa washukiwa wengine katika wiki na miezi ijayo.