Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amepinga madai kwamba visa vya utekaji nyara nchini vimeongezeka tangu mwaka 2024, akisisitiza kuwa takwimu zinaonyesha kupungua kwa matukio hayo tangu serikali ya Rais William Ruto ilipoingia mamlakani mwaka 2022.

Akizungumza mbele ya Bunge la Taifa Jumatano, Novemba 4, Murkomen amesema madai ya kuongezeka kwa visa vya utekaji nyara hayana msingi, akidai kuwa serikali imejitolea kutokomeza mauaji ya kiholela na utekaji nyara.

Murkomen amesema serikali ya sasa imefanikiwa kudhibiti matukio ya watu kutoweka kwa lazima, akilinganisha hali ya sasa na utawala uliopita ambapo, kwa mujibu wake, visa vya miili kupatikana katika Mto Yala na watu kutoweka vilikuwa vimeenea.

“Dai kwamba visa vya utekaji nyara vimeongezeka tangu 2024 ni la uongo. Kinyume chake, takwimu zinaonyesha kuwa tangu tulipoingia mamlakani mwaka 2022, hakujakuwa na miili iliyokuwa ikielea katika Mto Yala kama ilivyokuwa awali,” alisema Murkomen.

Aliongeza kuwa serikali iliahidi wakati wa kampeni kukomesha mauaji ya kiholela na utekaji nyara, akisema matukio yote ya hivi karibuni yanayoripotiwa yanachunguzwa na waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria.

Hata hivyo, waziri huyo alidai kuwa baadhi ya matukio yanayoripotiwa kama utekaji nyara huenda yakawa yamepangwa na wahusika wenyewe kwa lengo la kupata huruma ya umma, kujipatia umaarufu au kusukuma ajenda zao za kisiasa.

Murkomen pia alionya dhidi ya kuchanganya kukamatwa kwa viongozi wa kisiasa na visa vya utekaji nyara, akitaja kukamatwa kwa Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji kwa tuhuma za wizi na uchochezi kuwa jambo lisilopaswa kuwasilishwa kama utekaji nyara.

Kauli ya Murkomen inajiri huku kukiwa na wasiwasi mkubwa wa umma kuhusu watu wanaoripotiwa kutoweka au kutekwa nyara nchini, hali iliyozua maandamano, malalamiko ya kisheria na ukosoaji kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini (KNCHR) hivi majuzi ilirekodi visa vipya 46 vya watu kutoweka kwa lazima katika ripoti ya mfumo wa fidia iliyowasilishwa kwa Rais Ruto Juni 2026.

Tume hiyo ilisema visa vingi vinahusisha waandamanaji waliowekwa kizuizini bila mawasiliano na kuteswa, huku ikitaka serikali kufichua mahali walipo watu ambao bado hawajulikani waliko.

Murkomen amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuhakikisha usalama wa wananchi na kuchukua hatua dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na uhalifu.