Katibu Mkuu katika Wizara ya Afya nchini Kenya, Mary Muthoni, ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Nne cha Chanjo Barani Afrika (Continental Immunisation Task Force 4).

Hatua hii inatarajiwa kuimarisha nafasi ya Kenya katika kuongoza juhudi za kupanua huduma za chanjo barani humo.

Uteuzi huo ulifanywa na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), huku Muthoni akisema nafasi hiyo itaiwezesha Kenya kushiriki kikamilifu katika kuunda vipaumbele vya bara hili kuhusu chanjo na kuharakisha utekelezaji wa Mkakati wa Chanjo wa Afrika wa mwaka 2026 hadi 2030.

Muthoni alisema atajikita katika kuoanisha ushirikiano wa wadau na vipaumbele vya kitaifa, kuimarisha ufadhili endelevu wa mipango ya chanjo, kuondoa vikwazo vinavyozuia upatikanaji wa chanjo na kuhakikisha uwajibikaji katika kufanikisha malengo yaliyowekwa.

Alimshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Dkt Jean Kaseya, kwa kumwamini na kumpa jukumu hilo, akiahidi kushirikiana na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Africa CDC pamoja na washirika wengine kuboresha upatikanaji wa chanjo kwa usawa.

Alisema ushirikiano huo pia utasaidia kuimarisha mifumo ya afya ya umma katika bara hili, hasa kwa jamii zilizo katika mazingira magumu na maeneo ambayo huduma za chanjo bado hazijafikia watu wengi.

Uteuzi huo unajiri wakati mataifa ya Afrika yakiongeza juhudi za kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, programu za chanjo na maandalizi ya kukabiliana na dharura za kiafya, kufuatia vitisho vinavyoendelea kujitokeza, vikiwemo milipuko ya Ebola.

Africa CDC ina jukumu muhimu la kuratibu juhudi za mataifa ya Afrika katika kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza kupitia ushirikiano na taasisi za afya za kitaifa, Shirika la Afya Duniani (WHO) na washirika wengine.

Wakati wa milipuko ya Ebola, taasisi hiyo husaidia kuratibu shughuli za dharura, kupeleka wataalamu wa afya, kuimarisha uwezo wa maabara na mifumo ya ufuatiliaji, pamoja na kuhamasisha rasilimali zinazohitajika kudhibiti maambukizi.

Pia, inasaidia kuboresha udhibiti wa maambukizi katika hospitali, ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa na utoaji wa taarifa sahihi kwa umma.

Changamoto za usafiri wa watu kuvuka mipaka zinaongeza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kuzuia kuenea kwa magonjwa hatari.

Aidha, ufadhili endelevu wa chanjo unabaki kuwa kipaumbele, huku nchi za Afrika zikilenga kupunguza utegemezi wa fedha kutoka nje na kuhakikisha programu za kawaida za chanjo zinaendelea kutekelezwa.

Kupitia wadhifa huo, Muthoni anatarajiwa kushirikiana na wadau wa bara hili kuziba mapengo katika utoaji wa chanjo na kujenga mifumo imara ya afya inayoweza kukabiliana na milipuko ya magonjwa siku zijazo.