Mgogoro wa uongozi ndani ya Shirikisho la Soka nchini Kenya (FKF) umechukua sura mpya baada ya Makamu wa Rais wa shirikisho hilo, McDonald Mariga, pamoja na wajumbe wengine sita wa Kamati Kuu ya Utendaji (NEC), kuondolewa madarakani kupitia mkutano maalum wa wajumbe wa shirikisho hilo uliofanyika Meru.
Hatua hiyo imeongeza uzito wa mvutano wa uongozi uliodumu kwa miezi kadhaa kati ya Mariga na Rais wa FKF, Hussein Mohammed, huku mustakabali wa usimamizi wa soka nchini ukiendelea kuibua maswali kuhusu utulivu wa shirikisho hilo.
Mkutano huo maalum wa General Assembly ulifanyika katika Hoteli ya Three Steers mjini Meru, ukiwa na ajenda ya kujadili mwenendo wa wajumbe saba wa NEC ambao wamekuwa katikati ya mzozo wa kiuongozi ndani ya shirikisho hilo.
Wengine walioondolewa ni Kerubo Momanyi, Dan Shikanda, Gabriel Mghendi, Collins Opiyo Kalee, Robert Macharia na Bernard Lagat.
Kuondolewa kwao kunafuatia mvutano uliozidi kushika kasi ndani ya FKF tangu Aprili mwaka huu, wakati wajumbe tisa kati ya 14 wa NEC walipopitisha azimio la kumtaka Hussein Mohammed kuachia nafasi yake kwa muda ili kupisha uchunguzi kuhusu madai ya matumizi mabaya ya fedha za shilingi milioni 42.48 zilizohusishwa na maandalizi ya mashindano ya CHAN 2024.
Katika azimio hilo, Mariga alipendekezwa kuchukua nafasi ya kaimu rais wa shirikisho hilo, hatua iliyozua mvutano zaidi kuhusu uhalali wa mchakato huo. Hata hivyo, FIFA ilipinga hatua ya kuwasimamisha viongozi hao, ikieleza kuwa utaratibu uliotumika haukuzingatia katiba ya FKF.
Kwa upande mwingine, Hussein Mohammed naye amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kuondolewa madarakani baada ya wawakilishi wa General Assembly kumtaka ajibu tuhuma sita zinazohusu utawala, usimamizi wa fedha, uteuzi wa viongozi na madai ya kuingilia shughuli za ligi.
Mzozo huo umeendelea kugawanya viongozi na wadau wa soka, huku pande tofauti zikionekana kutetea misimamo yao kuhusu namna shirikisho linavyopaswa kuendeshwa.
Mkutano wa Meru pia uliandamana na hali ya sintofahamu baada ya mvutano na vurugu kuripotiwa katika eneo la mkutano, hali iliyolazimu polisi kuingilia kati na kutumia gesi ya kutoa machozi kutawanya baadhi ya waliokuwa wamekusanyika.
Kuondolewa kwa Mariga na wenzake kunafungua ukurasa mwingine katika mgogoro wa FKF, wakati Kenya ikiendelea na maandalizi ya kuandaa kwa pamoja michuano ya AFCON 2027 pamoja na Tanzania na Uganda.
Sasa macho yanaelekezwa kwa hatua zitakazofuata ndani ya shirikisho hilo na namna uongozi utakavyoshughulikia mgawanyiko uliopo ili kurejesha utulivu katika usimamizi wa soka nchini.









