Mahakama nchini Kenya imejibu vikali ukosoaji unaoelekezwa kwa idara ya mahakama kuhusu namna inavyoshughulikia kesi za utekaji nyara na watu kutoweka katika mazingira yasiyoeleweka, ikisisitiza kuwa haiwezi kulaumiwa kwa kushindwa kutekeleza majukumu ya polisi na vyombo vya usalama.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Novemba 6, 2026, msemaji wa Idara ya Mahakama, Paul Ndemo, alisema taasisi hiyo imekuwa ikifuatilia mijadala ya umma kufuatia makala iliyochapishwa na gazeti moja la humu nchini ikihoji namna mahakama inavyoshughulikia visa vya utekaji na madai ya kutowajibishwa kwa maafisa wa usalama.

Ndemo alisema mahakama inatambua nafasi ya vyombo vya habari katika kuisimamia serikali, lakini akaonya kuwa uhuru wa vyombo hivyo unapaswa kuambatana na uwajibikaji, usahihi na uelewa wa majukumu ya kila taasisi.

Alifafanua kuwa mahakama ni taasisi huru inayosikiliza na kuamua migogoro kwa kuzingatia Katiba, sheria na ushahidi unaowasilishwa mbele yake, badala ya kufanya uchunguzi wa uhalifu, kuendesha mashtaka au kutekeleza operesheni za kiusalama.

Hata hivyo, mahakama imelaani vikali vitendo vya utekaji nyara, watu kutoweka kwa lazima na ukiukaji mwingine wa haki za kikatiba, ikisema imekuwa ikitumia mamlaka yake kulinda haki za wananchi kupitia taratibu za kisheria.

Miongoni mwa taratibu hizo ni maombi ya habeas corpus, ambayo huruhusu mahakama kuagiza mamlaka husika kumfikisha mtu anayeshikiliwa mbele yake na kueleza sababu za kuzuiliwa kwake au kutoa taarifa kuhusu aliko.

Ndemo alisisitiza kuwa maagizo yanayotolewa na mahakama katika kesi hizo yana nguvu ya kisheria na yanapaswa kutekelezwa na kila mtu au taasisi, zikiwemo idara za serikali na vyombo vya usalama.

Alisema jukumu la kutii maagizo hayo liko kwa wale walioelekezwa kuyatekeleza.

Aidha, aliitaka sekta ya habari kutofautisha majukumu ya mahakama na yale ya polisi, wachunguzi na waendesha mashtaka, akionya kuwa kuilaumu mahakama kwa mapungufu ya taasisi nyingine kunaweza kupotosha umma kuhusu mahali ambapo uwajibikaji unapaswa kuwekwa.

Kauli hiyo inajiri wakati ambapo masuala ya watu kutoweka na madai ya utekaji yameendelea kuzua mjadala nchini, huku kesi ya wakili Abshir Ahmedsadak Abdi, aliyeripotiwa kutoweka baada ya kutekwa mnamo Novemba 1, ikiangazia upya wito wa kutaka vyombo vya usalama vifichue aliko.

Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kimekuwa kikishinikiza hatua zichukuliwe kuhakikisha Abshir anapatikana salama na waliohusika wanawajibishwa.

Mjadala huo umeongeza shinikizo kwa taasisi za serikali kueleza hatua zinazochukuliwa kulinda haki za raia.

Mahakama imesema iko tayari kukosolewa, lakini ikataka ukosoaji huo uzingatie ukweli na mipaka ya kikatiba ya kila taasisi, ili kuimarisha haki na imani ya umma katika utawala wa sheria.