Mwanaharakati mashuhuri wa demokrasia nchini Hong Kong, Joshua Wong, amehukumiwa kifungo cha miaka 10 zaidi gerezani, katika hatua inayozidi kuongeza muda wake wa kukaa korokoroni kutokana na shughuli zake za kisiasa.
Wong, ambaye amekuwa mmoja wa sura zinazotambulika zaidi katika harakati za kutetea demokrasia na uhuru wa kisiasa Hong Kong, amekuwa akikabiliwa na kesi mbalimbali zinazohusiana na usalama wa taifa na maandamano ya kupinga serikali.
Katika hukumu iliyotolewa Alhamisi, Novemba 5, 2026, mahakama ilimpata Wong na washirika wake na hatia ya kula njama ya kushirikiana na mataifa ya kigeni kuchukua hatua dhidi ya China na utawala wa Hong Kong.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa Wong alishirikiana na mwanaharakati Nathan Law, ambaye anaishi uhamishoni, pamoja na washirika wengine, kushawishi mataifa ya kigeni, taasisi na watu binafsi kuweka vikwazo dhidi ya China na Hong Kong.
Inadaiwa kuwa shughuli hizo zilifanyika kati ya Julai na Novemba 2020, baada ya China kutekeleza sheria mpya ya usalama wa taifa katika eneo hilo.
Jaji William Tam aliamua kuwa kosa hilo lilikuwa zito, akitaja miaka 13 kuwa msingi wa hukumu kabla ya kupunguza miaka mitatu kutokana na Wong kukiri mashtaka na kuzingatia sababu nyingine za kupunguziwa adhabu.
Hata hivyo, hukumu hiyo mpya itaongeza muda wa mwanaharakati huyo gerezani, licha ya kuwa tayari anatumikia kifungo cha miaka minne na miezi minane kutokana na kesi nyingine ya kuchochea mapinduzi dhidi ya serikali.
Wong alikuwa anatarajiwa kuachiliwa huru Januari 2027 baada ya kukamilisha kifungo chake cha awali, lakini hukumu hiyo mpya inamaanisha kuwa huenda akabaki gerezani hadi mwaka 2036.
Wong alijipatia umaarufu akiwa kijana kupitia maandamano ya mwaka 2014 yaliyojulikana kama Umbrella Movement, yaliyolenga kutaka mageuzi ya kidemokrasia na mfumo wa uchaguzi Hong Kong.
Baadaye, alikuwa miongoni mwa viongozi wa maandamano makubwa ya mwaka 2019 yaliyopinga ushawishi wa Beijing katika masuala ya utawala wa eneo hilo.
Mwaka 2020, China ilitekeleza sheria kali ya usalama wa taifa iliyolenga kukabiliana na kile serikali ilichokitaja kuwa vitisho dhidi ya usalama na utulivu wa Hong Kong.
Sheria hiyo imekuwa ikitumiwa kuwafungulia mashtaka wanaharakati na viongozi mbalimbali wa upinzani, huku hatua hiyo ikikabiliwa na ukosoaji kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Shirika la Human Rights Watch limekosoa hukumu mpya dhidi ya Wong, likiitaja kuwa ya kikatili na isiyo ya haki.
Wong, ambaye alitimiza miaka 30 mwezi Oktoba, amekuwa gerezani kwa karibu miaka sita kutokana na kesi mbalimbali zinazohusiana na harakati zake za kisiasa.









