Shirika la Wafamasia nchini Kenya (PSK) limeibua wasiwasi kuhusu madai yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii yanayohimiza matumizi ya dawa ya Cetirizine kwa lengo la kubana uke, likionya kuwa matumizi yasiyofaa ya dawa yanaweza kuhatarisha afya ya watumiaji.

Katika taarifa yake, PSK imesema imebaini mijadala inayopigia debe matumizi ya dawa hiyo, ikiwemo madai yanayowahimiza wanawake kuingiza tembe za Cetirizine ukeni kwa madai kuwa zinaweza kusaidia kukaza misuli ya uke.

Shirika hilo, ambalo ni bodi ya kitaaluma inayowakilisha wafamasia nchini Kenya, limesema madai hayo yanapotosha umma kuhusu matumizi sahihi ya dawa na yanahitaji kushughulikiwa ili kuzuia wananchi kupotoshwa na taarifa zisizothibitishwa kisayansi.

PSK imefafanua kuwa Cetirizine ni dawa inayotumika kupunguza dalili za mzio kama vile kupiga chafya, mafua ya mzio, kuwashwa kwa ngozi na macho kutoa machozi.

Dawa hiyo hufanya kazi kwa kuzuia athari za histamine, kemikali inayozalishwa na mwili wakati wa mwitikio wa mzio na kusababisha dalili mbalimbali za mzio.

Hata hivyo, matumizi ya Cetirizine kwa lengo la kubana uke hayana msingi wa kitabibu uliothibitishwa, huku kuingiza tembe hizo ukeni kukiwa si njia iliyoidhinishwa ya kuitumia dawa hiyo.

Wataalamu wa afya wanaonya kuwa kuingiza dawa ambazo hazijatengenezwa kwa matumizi ya ukeni kunaweza kusababisha muwasho, kuathiri tishu laini za uke na kuvuruga uwiano wa kawaida wa mazingira ya uke.

PSK imesisitiza kuwa dawa zinapaswa kutumiwa kwa madhumuni yaliyokusudiwa kitabibu na kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, badala ya kufuata ushauri unaosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Aidha, wananchi wametakiwa kuwa waangalifu wanapokutana na madai yanayohusisha matumizi ya dawa kwa njia zisizo za kawaida, hasa pale ambapo madai hayo hayajaungwa mkono na ushahidi wa kisayansi.

Shirika hilo pia limekumbusha umuhimu wa kushauriana na wafamasia au wahudumu wengine wa afya kabla ya kutumia dawa yoyote kwa madhumuni tofauti na yale iliyoidhinishwa.

Onyo hilo linajiri wakati ambapo mitandao ya kijamii imekuwa chanzo cha taarifa mbalimbali za afya, hali inayozua wasiwasi kuhusu kasi ya kusambaa kwa taarifa potofu zinazoweza kuwafanya wananchi kufanya maamuzi yanayohatarisha afya zao.