Wabunge wawili waandamizi wa Marekani wamepinga uamuzi wa utawala wa Rais Donald Trump wa kuiondoa Afrika Kusini kwenye mpango wa biashara wa African Growth and Opportunity Act (AGOA).

Aidha wameonya kuwa hatua hiyo inaweza kudhoofisha maslahi ya kiuchumi ya Marekani barani Afrika na kuipa China nafasi kubwa zaidi ya kupanua ushawishi wake katika eneo hilo.

Wabunge hao, Gregory Meeks na Jeanne Shaheen, wamesema hatua ya kuitenga Afrika Kusini kwenye mpango huo huenda ikawa na madhara makubwa kwa uhusiano wa kibiashara kati ya Washington na mataifa ya Afrika.

Katika taarifa ya pamoja, viongozi hao wameeleza kuwa AGOA imekuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Marekani na Afrika, huku ikiwezesha kampuni za Marekani kupata fursa za kibiashara na kuchochea ukuaji wa uchumi katika mataifa yanayonufaika na mpango huo.

Wamesema kuwa kuondolewa kwa Afrika Kusini kunaweza kudhoofisha juhudi za Marekani za kudumisha nafasi yake kama mshirika muhimu wa kibiashara barani Afrika, wakati ambapo China inaendelea kupanua ushirikiano wake wa kiuchumi na nchi mbalimbali za eneo hilo.

Kwa mujibu wa wabunge hao, uamuzi huo unaweza kuacha pengo ambalo mataifa mengine, hususan China, yanaweza kulitumia kuimarisha ushawishi wao katika masuala ya biashara na uwekezaji barani Afrika.

Aidha, wameonya kuwa hatua hiyo inaweza kuvuruga minyororo ya usambazaji bidhaa kati ya Marekani na Afrika Kusini, hali inayoweza kuathiri wazalishaji wa Marekani pamoja na biashara zinazotegemea masoko ya nchi hiyo.

Meeks na Shaheen wamebainisha kuwa manufaa ya AGOA hayaishii kwa mataifa ya Afrika pekee, bali pia yana umuhimu mkubwa kwa kampuni na wafanyabiashara wa Marekani wanaotegemea fursa zinazotokana na ushirikiano huo.

Kutokana na hali hiyo, wameitaka Ofisi ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani (USTR) pamoja na Ikulu ya White House kutumia kipindi cha siku 60 cha taarifa rasmi kufanya mazungumzo na serikali ya Afrika Kusini.

Wabunge hao wanataka mazungumzo hayo yatumiwe kutafuta suluhu kuhusu masuala yanayohusiana na ustahiki wa Afrika Kusini kuendelea kunufaika na mpango huo, badala ya kuchukua hatua zinazoweza kuzorotesha uhusiano wa muda mrefu wa kibiashara.

AGOA ni mpango wa Marekani unaolenga kupanua fursa za biashara kwa mataifa ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuyapa bidhaa zinazostahiki nafasi ya kuingia katika soko la Marekani kwa masharti maalumu.

Mpango huo pia unalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kukuza ajira na kuongeza uwekezaji kati ya Marekani na mataifa ya Afrika.