Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, ameanza kuonyesha tofauti za msimamo na Rais Donald Trump kuhusu sera za kigeni, kufuatia kushindwa kwa chama cha Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula (Midterm Elections) uliofanyika Novemba 3, 2026.
Vance anadaiwa kutafuta kuunda muungano mpya wa kisiasa unaolenga kuwavutia tena wafuasi wa Trump ambao hawajaridhishwa na baadhi ya maamuzi ya utawala wa sasa, hasa kuhusu vita vya Iran na uhusiano wa Marekani na Israel.
Kwa mujibu wa taarifa ya kipekee ya Fox News Digital, hatua hiyo inajiri baada ya mkutano uliofanyika katika Ikulu ya White House Jumatano asubuhi, Novemba 4, ambao chanzo kimoja kilisema ulilenga kuratibu ujumbe wa maafisa wa serikali kufuatia matokeo ya uchaguzi huo.
Hata hivyo, chanzo kingine kilichoelezwa na chombo hicho kilisema mkutano huo ulikuwa wa kawaida wa maafisa wakuu wa serikali.
Baada ya mkutano huo, Vance alichapisha ujumbe mrefu kwenye mtandao wa X, akieleza sababu alizoamini zilichangia chama cha Republican kupata matokeo mabaya katika uchaguzi huo.
Vance alilaumu vita vinavyoendelea nchini Iran, akisema kuwa mzozo huo ndio sababu kuu iliyochangia chama chake kupoteza uungwaji mkono wa wapiga kura.
"Sababu iliyotufanya tushindwe ni vita. Rais mwenyewe alisema hivyo jana usiku," alisema Vance katika ujumbe wake.
Aidha, alionya kuwa chama hicho kinahitaji kukabiliana na hali hiyo kwa uaminifu badala ya kupuuza sababu zilizochangia kushindwa kwake.
Katika ujumbe huo, Vance alitaja maeneo manne ambayo anasema yanafaa kupewa kipaumbele ili kurejesha imani ya wapiga kura.
Maeneo hayo ni pamoja na kumaliza vita vya Iran, kukabiliana na kupanda kwa gharama ya maisha na mfumuko wa bei, kutanguliza maslahi ya Marekani pamoja na kubadilisha namna nchi hiyo inavyoshirikiana na Israel.
Afisa mmoja wa utawala wa Trump aliiambia vyombo vya habari kuwa masuala hayo yanaunda ajenda ya kile kinachotajwa kama 'New Right', kundi la kisiasa linalolenga kuunganisha wahafidhina wanaounga mkono sera za 'America First'.
Kundi hilo linajumuisha baadhi ya wafuasi wa Trump wanaoamini kuwa Marekani imejihusisha kupita kiasi katika migogoro ya kimataifa na kuwa uhusiano wake na Israel unahitaji kutathminiwa upya.
Afisa huyo alifafanua kuwa ujumbe wa Vance hauashirii moja kwa moja kujitenga na Trump, bali unalenga kuwafikia wapiga kura wanaomuunga mkono rais huyo lakini hawaridhishwi na sera zake za kigeni.
Hatua hiyo inajiri huku Vance akitajwa kuwa mmoja wa wanasiasa wanaoweza kuwania urais wa Marekani katika uchaguzi wa 2028, ingawa hajatangaza rasmi azma hiyo.









