Serikali ya Ecuador imetangaza amri ya kutotoka nje wakati wa usiku katika mikoa mitano nchini humo.
Hatua hiyo itaanza kutekelezwa Jumapili, Novemba 1, hadi Jumanne, Novemba 10, 2026, kufuatia agizo la Rais kupitia Amri ya Utendaji nambari 519.
Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa kila siku kuanzia saa sita usiku hadi saa kumi na moja alfajiri katika mikoa ya Guayas, Manabí, Los Ríos, El Oro na Esmeraldas.
Hatua hiyo inakuja wakati serikali ya Rais Daniel Noboa ikiendelea kukabiliana na changamoto ya uhalifu unaohusishwa na makundi ya kihalifu yaliyopangwa, ambayo yamekuwa yakichangia kuzorota kwa usalama katika baadhi ya maeneo nchini humo.
Katika kipindi cha marufuku hiyo, vikosi vya usalama vinatarajiwa kuimarisha doria na operesheni za kukabiliana na wahalifu, huku mamlaka zikidhibiti mienendo ya watu na magari katika maeneo yaliyoathiriwa.
Marufuku hiyo pia inatekelezwa wakati wa kipindi cha likizo zinazohusishwa na Siku ya Wafu na maadhimisho ya uhuru wa Cuenca, ambapo usafiri wa watu ndani ya nchi unaweza kuongezeka.
Serikali ya Marekani imewaonya raia wake walioko Ecuador kuepuka safari zisizo za lazima katika maeneo yaliyoathiriwa wakati wa saa zilizowekwa za marufuku hiyo.
Wasafiri wenye safari za ndege zinazowasili au kuondoka katika kipindi hicho wameshauriwa kuwasiliana na mashirika yao ya ndege na mamlaka husika ili kufahamu masharti ya usafiri na kupata ruhusa zinazohitajika.
Aidha, huduma za usafiri wa umma, teksi na magari yanayotumia programu za simu zinaweza kuathirika kutokana na utekelezaji wa amri hiyo, hali inayowataka wasafiri kupanga safari zao mapema.
Hata hivyo, hali za dharura, zikiwemo zinazohitaji matibabu ya haraka au zinazohatarisha maisha na usalama wa watu, zinaweza kushughulikiwa kwa kuzingatia masharti yatakayowekwa na mamlaka za nchi hiyo.
Ecuador imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya usalama kutokana na makundi ya kihalifu yanayohusishwa na biashara haramu ya dawa za kulevya na uhalifu mwingine uliopangwa.
Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kiusalama, zikiwemo operesheni za polisi na wanajeshi, ili kudhibiti shughuli za makundi hayo na kurejesha utulivu.
Wakazi na wageni wametakiwa kufuatilia matangazo rasmi ya serikali, kutii maagizo ya maafisa wa usalama na kuepuka maeneo yanayoweza kuwa hatarishi katika kipindi chote ambacho marufuku hiyo itakuwa ikitekelezwa.









