Ethiopia imepokea ndege 12 za kivita aina ya Su-35 kutoka Urusi, katika hatua inayolenga kuimarisha uwezo wake wa kijeshi wakati mvutano wa kiusalama ukiendelea katika eneo la Tigray, kaskazini mwa nchi hiyo, karibu na mpaka wa Eritrea.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, amesema kuwasili kwa ndege hizo ni hatua muhimu katika juhudi za serikali yake kuimarisha ulinzi wa taifa dhidi ya vitisho vinavyoweza kuhatarisha usalama wake.

Abiy ametoa kauli hiyo akiwa mjini Moscow, Urusi, ambako anahudhuria mkutano wa kilele wa Urusi na Afrika.

Amesema ununuzi wa ndege hizo unatokana na ushirikiano wa muda mrefu wa kijeshi kati ya Ethiopia na Urusi.

Kiongozi huyo ameeleza kuwa mataifa hayo mawili yalitia saini mkataba wa ushirikiano wa ulinzi miaka kadhaa iliyopita, na kwamba ndege hizo zimewasili mapema kuliko muda uliokuwa umepangwa.

Aidha, Abiy amesema Ethiopia inapanga kununua mifumo minne ya ulinzi wa anga aina ya S-400 kutoka Urusi, hatua ambayo inaweza kuimarisha zaidi uwezo wa nchi hiyo kukabiliana na mashambulizi ya angani.

Mifumo ya S-400 hutengenezwa na Urusi na imeundwa kutambua na kukabiliana na vitisho mbalimbali vya angani, vikiwemo ndege za kivita na makombora.

Pia amemtaja Rais wa Urusi, Vladimir Putin, kama rafiki wa karibu wa Ethiopia, akionyesha umuhimu wa uhusiano wa kidiplomasia na kijeshi kati ya mataifa hayo mawili.

Ushirikiano huo umekuwa ukiimarika katika miaka ya hivi karibuni, huku nchi hizo zikitia saini mikataba mbalimbali inayohusisha mafunzo ya wanajeshi, teknolojia ya kijeshi na masuala ya ulinzi.

Mwaka 2021, Ethiopia na Urusi zilitia saini mkataba uliolenga kuimarisha ushirikiano wa kijeshi, ikiwemo kutoa mafunzo kwa wanajeshi na kuboresha teknolojia inayotumiwa na vikosi vya ulinzi.

Wakati huo huo, hali ya usalama katika eneo la Tigray inaendelea kuwa suala muhimu kwa serikali ya Ethiopia, kutokana na historia ya mapigano yaliyosababisha vifo, uharibifu wa miundombinu na kuwakosesha maelfu ya watu makazi.

Eneo hilo lilikuwa kitovu cha vita vilivyoanza mwaka 2020 kati ya serikali ya shirikisho na vikosi vya Tigray, kabla ya makubaliano ya kusitisha mapigano kufikiwa mwaka 2022.

Kupokelewa kwa ndege hizo kunatarajiwa kuibua mjadala kuhusu ongezeko la matumizi ya kijeshi katika Pembe ya Afrika, eneo ambalo kwa muda mrefu limekabiliwa na changamoto za usalama na mivutano ya kisiasa.

Hata hivyo, haijabainika mara moja ni lini Ethiopia itakamilisha ununuzi wa mifumo ya S-400 au gharama kamili ya makubaliano hayo ya kijeshi.