Waziri wa Elimu nchini Korea Kusini, Choi Kyo-jin, amejiuzulu kufuatia kashfa ya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa iliyohusisha matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (AI), huku hatua za dharura zilizochukuliwa na serikali kudhibiti udanganyifu huo zikizua mkanganyiko miongoni mwa wanafunzi na walimu.

Choi alitangaza uamuzi wake Jumapili, Novemba 22, 2026, akisema anawajibika kwa usumbufu uliosababishwa na mabadiliko ya ghafla ya kanuni za usalama kabla ya mtihani wa kitaifa wa kujiunga na vyuo vikuu, unaojulikana kama Suneung.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Habari la Yonhap, Rais Lee Jae Myung alikubali ombi la waziri huyo la kujiuzulu muda mfupi baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo.

Katika kueleza sababu za kujiuzulu, Choi alisema wizara yake ilishindwa kujiandaa mapema kukabiliana na changamoto ya udanganyifu unaotumia teknolojia mpya.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na mamlaka ni kutuma jumbe za tahadhari kwenye simu za mkononi kote nchini wakati mtihani ukiendelea, pamoja na kuwakagua watahiniwa ili kubaini vifaa vya kielektroniki vilivyofichwa kwenye mavazi na miwani.

Hatua hizo zilichukuliwa baada ya kuibuka kwa taarifa za watahiniwa kutumia kamera ndogo, simu na mifumo ya AI kupata majibu ya mitihani.

Wasiwasi kuhusu udanganyifu huo uliongezeka baada ya Han Won-seok, aliyekuwa amepata alama za juu zaidi katika mtihani wa kitaifa wa wahasibu wa kodi mwezi Aprili, kukiri kutumia vifaa vya kisasa kudanganya.

Han, mwenye umri wa miaka 34, alieleza kuwa alitumia kamera ndogo iliyofichwa kupiga picha za maswali ya mtihani na kuyatuma kwenye mfumo wa AI ili kupata majibu. Baadaye alitumia simu yake ya mkononi kukagua majibu hayo.

Inaripotiwa kuwa alikuwa amekosea swali moja pekee kati ya maswali 160, jambo lililozua mashaka kuhusu matokeo yake kabla ya kukiri udanganyifu huo.

Kukiri kwake kulisababisha serikali kuharakisha maandalizi ya kukabiliana na udanganyifu katika mtihani wa Suneung uliofanyika Alhamisi iliyopita, Novemba 19, huku takribani wanafunzi 500,000 wakishiriki.

Katika mtihani huo, mamlaka zilituma jumbe tatu za tahadhari kwa simu za mkononi kote nchini kati ya saa mbili asubuhi na saa tisa alasiri kwa saa za Korea Kusini, ikiwa ni mara ya kwanza mfumo wa tahadhari za majanga kutumiwa katika operesheni ya kubaini wanafunzi wanaodanganya.

Aidha, watahiniwa walitakiwa kufunika vifungo vya mashati na makoti yao kwa vibandiko ili kuzuia matumizi ya kamera ndogo zilizofichwa, huku miwani na vifaa vingine vikikaguliwa kwa makini.

Hata hivyo, hatua hizo zilikosolewa na baadhi ya wanafunzi na walimu wakisema zilisababisha hofu na mkanganyiko usio wa lazima wakati wa mtihani ambao tayari una presha kubwa.

Wizara ya Elimu ilisema watahiniwa 111 walibainika kuwa na vifaa vya kielektroniki visivyoruhusiwa wakati wa mtihani wa mwaka huu.

Mtihani wa Suneung ni miongoni mwa mitihani muhimu zaidi nchini Korea Kusini, kwa kuwa matokeo yake yana nafasi kubwa katika kuamua vyuo ambavyo wanafunzi watajiunga navyo na fursa zao za baadaye za ajira.

Rais Lee amekuwa akitaka kufanyiwa mageuzi mfumo wa sasa wa mitihani ili kupunguza changamoto zinazowakabili wanafunzi na kuhakikisha mchakato wa kujiunga na vyuo vikuu unakuwa wa haki.

Kwa sasa, serikali inatarajiwa kuendelea kuchunguza mianya ya udanganyifu unaotumia teknolojia ya kisasa huku mchakato wa kumpata mrithi wa Choi ukiendelea.