Kibera Yageuka Majivu, Zaidi Ya Familia 20 Zapoteza Makazi
Zaidi ya kaya 20 zimebaki bila makazi kufuatia moto mkubwa ulioteketeza zaidi ya nyumba 20 katika eneo la mabanda la Kibera jijini Nairobi usiku wa kuamkia leo,Jumanne,Novemba 24,2026.
Hali hiyo imewaacha waathiriwa wakikadiria hasara baada ya kupoteza makazi na mali zao.
Aidha moto ulizuka katika eneo hilo na kusambaa kwa kasi hadi kwenye nyumba za jirani, hali iliyosababisha wakazi wengi kushindwa kuokoa mali zao huku wakijitahidi kujinusuru na miali ya moto.
Baadhi ya waathiriwa wamesema moto huo ulisababisha uharibifu mkubwa, huku familia kadhaa zikilazimika kutumia usiku huo bila mahali pa kujisitiri baada ya nyumba zao kuteketea.
Wakazi walioathirika pia wameeleza kutoridhishwa na mwitikio wa timu za kukabiliana na majanga ya dharura, wakidai kuwa kikosi cha zimamoto kilichelewa kufika eneo la tukio, hali iliyowalazimu wakazi wenyewe kujitahidi kuudhibiti moto huo.
Kwa mujibu wa wakazi hao, kuchelewa kwa msaada wa dharura kulifanya juhudi za kuuzima moto kuwa ngumu zaidi, huku miali ikiendelea kusambaa na kuathiri nyumba nyingine.
Hata hivyo, haijabainika mara moja iwapo kuna watu waliojeruhiwa au kupoteza maisha katika mkasa huo, huku kiwango kamili cha hasara kikisubiriwa kufahamika.
Tukio hilo limewaacha waathiriwa katika hali ngumu, hasa familia zilizopoteza mahitaji muhimu ya kila siku yakiwemo mavazi, chakula, vitanda na vifaa vingine vya nyumbani.
Wakati huohuo, maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo na mazingira yaliyopelekea kutokea kwa mkasa huo.
Ingawa chanzo cha moto hakijabainika rasmi, wachunguzi wanatarajiwa kuchunguza uwezekano wa hitilafu za umeme au sababu nyingine zilizoweza kuchangia kuzuka kwake.
Mkasa huo umeibua tena wasiwasi kuhusu usalama wa wakazi wanaoishi katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu, ambako ukaribu wa nyumba unaweza kurahisisha moto kusambaa na kusababisha uharibifu mkubwa.
Kwa sasa, familia zilizoathirika zinakabiliwa na changamoto ya kupata makazi ya muda huku zikisubiri msaada wa kurejesha maisha yao baada ya kupoteza makazi yao.
Kumekuwa na visa vya moto kuteketeza mali ya wajasiriamali mara kwa mara huku vyanzo vikiwa haviwekwi wazi.









