Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameitaka Mahakama ya Juu nchini Kenya kutupilia mbali rufaa zilizowasilishwa na aliyekuwa afisa wa kwanza katika Ubalozi wa Venezuela, Dwight Sagaray, na raia wa Kenya Ahmed Mujivane Omido, huku akitaka hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela dhidi yao idumishwe kuhusiana na mauaji ya aliyekuwa balozi wa Venezuela nchini Kenya, Olga Fonseca Jimenez.
DPP amewasilisha ombi hilo mbele ya jopo la majaji wa Mahakama ya Juu likiongozwa na Jaji Smokin Wanjala, akisisitiza kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha uliothibitisha kuhusika kwa washukiwa hao katika mauaji hayo.
Upande wa mashtaka umesema kuwa hukumu dhidi ya wawili hao iliungwa mkono na ushahidi wa kimazingira uliokuwa na uzito mkubwa, ukiwaunganisha moja kwa moja na mauaji ya Fonseca.
Katika kujibu hoja kuhusu kinga ya kidiplomasia aliyokuwa nayo Sagaray, upande wa mashtaka umeeleza kuwa mamlaka za Venezuela zilikuwa zimewasilisha mawasiliano rasmi ya kusitisha utume wake wa kidiplomasia pamoja na kufuta pasipoti yake ya kidiplomasia.
Kwa mujibu wa DPP, hatua hiyo ilimaanisha kuwa majukumu yake ya kidiplomasia yalikuwa yamekamilika, hivyo hakuwa na kinga inayoweza kumzuia kufunguliwa mashtaka kutokana na vitendo vilivyodaiwa kutekelezwa nje ya majukumu yake rasmi.
DPP pia amepinga madai kwamba hukumu dhidi ya Sagaray ilitokana na uhusiano wake na watu wengine au nia ya kutaka kudhibiti shughuli za ubalozi huo pekee, akisema kuwa mahakama ilizingatia mkusanyiko wa ushahidi, ikiwemo mzozo kuhusu usimamizi wa Ubalozi wa Venezuela na matukio yaliyotangulia mauaji hayo.
Kuhusu Omido, upande wa mashtaka umesema hoja zake kuhusu dhamira ya pamoja katika kutekeleza uhalifu huo pamoja na ushahidi wake wa kujitetea kuwa hakuwa eneo la tukio hazina msingi wa kutosha kubatilisha hukumu.
DPP ameitaka Mahakama ya Juu kutambua kuwa rufaa hizo hazijaonyesha ukiukaji wowote wa kikatiba, kuzitupilia mbali pamoja na gharama za kesi na kudumisha vifungo vya miaka 20 jela dhidi ya wawili hao.
Sagaray na Omido walihukumiwa pamoja na Alex Sifuna Wanyonyi na Moses Kiprotich Kalya kuhusiana na mauaji ya Fonseca yaliyotekelezwa nyumbani kwake katika eneo la Runda, Nairobi, Julai 2012.
Mahakama ya Rufaa ilikuwa imethibitisha hukumu na adhabu hizo Machi 7, 2025, hatua iliyowasukuma wawili hao kuwasilisha rufaa katika Mahakama ya Juu.
Mahakama ya Juu inatarajiwa kutangaza tarehe ya kutoa uamuzi wake baadaye.









