Aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis,alipitia kipindi kigumu cha mgogoro wa kiroho wakati wa uongozi wake, ambapo alidai kuona maono ya Shetani na kuzimu huku akikabiliana na changamoto za namna ya kutumia mamlaka aliyokuwa nayo.
Maelezo hayo yameibuka kupitia shajara za marehemu Papa Francis zilizochapishwa hivi karibuni, zikifichua baadhi ya changamoto za ndani alizopitia katika kipindi chake cha uongozi wa Kanisa Katoliki.
Kwa mujibu wa taarifa ya vyombp vya habari, shajara hizo zinaeleza kuwa Papa Francis alipitia kipindi cha kutafakari kwa kina kuhusu nafasi yake kama kiongozi wa kiroho na namna alivyopaswa kutumia mamlaka aliyokabidhiwa.
Maelezo hayo yanaangazia mapambano yake ya ndani kuhusu uongozi, imani na wajibu mkubwa aliokuwa nao wa kuliongoza Kanisa Katoliki lenye waumini zaidi ya bilioni moja duniani.
Kitabu hicho chenye kurasa 160, kinachoitwa The Private Diary of Pope Francis, kimeandaliwa na Kardinali Víctor Manuel Fernández, mmoja wa wasaidizi wake wa karibu ambaye pia ni mkuu wa Idara ya Mafundisho ya Imani Vatican.
Papa Francis, ambaye aliongoza Kanisa Katoliki kwa miaka 12 hadi alipofariki Aprili 2025, aliandika shajara hizo kwa vipindi tofauti kati ya mwaka 1992 na Agosti 2024.
Katika maandishi hayo, Francis anaeleza matukio matatu aliyohisi kukutana na Shetani, mawili yakitokea alipokuwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires nchini Argentina na jingine mwaka 2021 alipokuwa tayari Papa.
Katika tukio la Januari 24, 2021, alisimulia jinsi alivyodai kumuona Shetani wakati wa mkutano na maafisa wa Vatican, akieleza kuwa sauti yake ilikuwa nzito na ya kutisha.
Shajara hizo pia zinaeleza kuwa mwaka 2018, baada ya kurejea kutoka ziara nchini Chile iliyozua mjadala kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto yaliyohusisha baadhi ya viongozi wa Kanisa, Francis aliandika kuwa alikuwa ameona lango la kuingia kuzimu.
Alieleza kuwa maono hayo yalimwogopesha kiasi cha kushika rozari yake na kuitumia katika maombi ili kupata faraja na ulinzi wa kiroho.
Ziara hiyo ya Chile ilikuwa imegubikwa na utata baada ya Francis kukosolewa kwa namna alivyoshughulikia madai dhidi ya baadhi ya viongozi wa kanisa. Baadaye alikiri kuwa alikuwa amepotoshwa kuhusu uzito wa tuhuma hizo na kwamba waathiriwa walikuwa na hoja za msingi.
Kwa mujibu wa Fernández, mgogoro mkubwa wa kiroho wa Papa ulianza Januari 2021 na kuendelea hadi mwishoni mwa mwaka 2022. Kipindi hicho kilihusisha changamoto za kiutawala, maamuzi magumu na mapambano dhidi ya kishawishi cha kutumia mamlaka kwa namna isiyofaa.
Fernández anasema Francis hatimaye alipata nafuu ya kiroho kwa kujikabidhi kwa rehema za Mungu na kutambua kuwa hakuwa na uwezo wa kutatua kila tatizo kwa nguvu zake mwenyewe.
Kitabu hicho kinatoa mtazamo wa ndani kuhusu maisha ya kiroho ya kiongozi huyo ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 88.









