Shirika la Ndege la Iraq (Iraqi Airways) limetangaza mpango wa kuuza ndege mbili aina ya Boeing 747 zilizotumiwa na Serikali ya Iraq wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Saddam Hussein, zikiwemo ndege iliyokuwa ikitumika kusafirisha viongozi wakuu wa serikali.
Miongoni mwa ndege hizo ni Boeing 747SP yenye usajili wa YI-ALM, iliyokadiriwa kuwa na thamani ya dola 900,000 za Marekani, ambayo imekuwa imeegeshwa katika Uwanja wa Ndege wa Tozeur–Nefta nchini Tunisia kwa takribani miaka 35.
Ndege hiyo ilihamishiwa nchini Tunisia Januari 1991, muda mfupi kabla ya kuanza kwa mashambulizi ya kijeshi yaliyohusishwa na Vita vya Ghuba, hatua iliyoiweka mbali na mapigano yaliyokuwa yakikumba Iraq wakati huo.
Ndege hiyo iliyojulikana kwa jina la Al-Qadissiya ilitengenezwa mwaka 1982 ikiwa na madhumuni maalumu ya kusafirisha viongozi waandamizi wa Serikali ya Iraq. Tofauti na ndege za kawaida za abiria, ilibuniwa ikiwa na mazingira ya kifahari yaliyolenga kukidhi mahitaji ya viongozi wakati wa safari za kikazi na shughuli rasmi.
Ndani ya ndege hiyo kulikuwa na chumba maalumu cha kulala, chumba cha mikutano pamoja na viti vilivyoweza kubadilishwa na kuwa vitanda, hali iliyoifanya kuwa na huduma zinazofanana na makazi ya kifahari angani.
Mbali na Boeing 747SP, Iraqi Airways pia imeweka sokoni ndege nyingine aina ya Boeing 747-200 yenye usajili wa YI-AGP, ambayo nayo imekadiriwa kuwa na thamani ya dola 900,000 za Marekani.
Kwa mujibu wa tangazo rasmi la shirika hilo, ndege hizo mbili zitauzwa katika hali zilivyo kwa sasa, bila kutolewa kwa dhamana yoyote kuhusu uwezo wake wa kiufundi au hali ya mifumo yake ya uendeshaji.
Hali hiyo ina maana kuwa wanunuzi watakaovutiwa na ndege hizo wanapaswa kuzingatia hali yake ya sasa kabla ya kuwasilisha ofa, ikizingatiwa kuwa zimekaa kwa muda mrefu bila kutumika katika shughuli za kawaida za usafiri wa anga.
Iraqi Airways imesema kamati ya mauzo itapokea na kutathmini ofa za wanunuzi katika Ubalozi wa Iraq nchini Tunisia kuanzia Desemba 21, 2026 hadi Januari 5, 2027.
Uamuzi wa kuuza ndege hizo unatoa fursa kwa wanunuzi wanaoweza kuvutiwa na ndege zenye historia ya kipekee, hasa kutokana na uhusiano wake na kipindi cha utawala wa Saddam Hussein na matukio ya Vita vya Ghuba vilivyoanza mwaka 1991.









