Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeeleza kuwa mpango wa kutangaza moja kwa moja shughuli za upigaji kura katika vituo vyote 50,000 nchini unaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa gharama za kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, amesema utekelezaji wa mpango huo unahitaji uwekezaji mkubwa katika vifaa vya kiteknolojia, rasilimali watu na maandalizi ya kiutendaji, wakati ambapo tayari Wakenya wameibua wasiwasi kuhusu gharama za uchaguzi ujao.

Akizungumza kuhusu pendekezo hilo, Ethekon ameeleza kuwa kuweka kamera katika kila kituo cha kupigia kura na kuhakikisha shughuli zote zinaonyeshwa mubashara kutahitaji fedha nyingi ambazo tume inapaswa kuzipangia bajeti.

amesema kuwa licha ya umuhimu wa teknolojia katika kuimarisha uwazi wa uchaguzi, utekelezaji wake hauwezi kufanyika bila maandalizi ya kutosha na tathmini ya gharama zitakazohusika.

Ethekon amesema kuwa kwa kuzingatia idadi ya vituo hivyo, IEBC italazimika kununua makumi ya maelfu ya kamera pamoja na vifaa vingine vitakavyowezesha matangazo ya moja kwa moja, hatua ambayo itahitaji fedha nyingi na muda wa kutosha kabla ya uchaguzi kufanyika.

Aidha, ameeleza kuwa tume italazimika kuajiri au kutenga wafanyakazi watakaopatiwa mafunzo maalumu ya kuendesha kamera hizo, kusimamia matangazo na kuhakikisha vifaa vinafanya kazi ipasavyo katika vituo vyote nchini.

Amesema zoezi hilo pia linahitaji muda wa kufanya manunuzi, majaribio ya vifaa na kuwasambaza waendeshaji katika maeneo mbalimbali, ikiwemo maeneo ya mbali ambako upatikanaji wa huduma za intaneti na umeme unaweza kuwa changamoto.

Msimamo huo unajiri wakati ambapo mjadala kuhusu uwazi wa uchaguzi wa mwaka 2027 unazidi kushika kasi, huku baadhi ya viongozi wa kisiasa na Wakenya wakitaka IEBC kuweka mifumo itakayowezesha wananchi kufuatilia moja kwa moja namna kura zinavyopigwa, kuhesabiwa na matokeo kutangazwa.

Hata hivyo, Ethekon amesisitiza kuwa uwepo wa wanahabari, mawakala wa vyama vya kisiasa na waangalizi wa uchaguzi katika vituo vya kupigia kura utasaidia kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa uwazi.

Amesema hakuna kizuizi kwa wanahabari kufika katika vituo vya kupigia kura au kushiriki katika ufuatiliaji wa shughuli za vituo vya kujumlishia kura katika maeneo bunge.

Akizungumzia suala la kujumlisha matokeo katika kituo cha kitaifa cha kujumlishia kura, Ethekon amesisitiza kuwa matokeo yanayotangazwa katika vituo vya kupigia kura ndiyo msingi wa matokeo rasmi, huku hatua zinazofuata katika ngazi ya kitaifa zikihusisha uthibitishaji na taratibu za kiutawala.

Mjadala huo unaibuka huku IEBC ikijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027, ambao utakuwa na nafasi muhimu katika kuamua uongozi wa nchi kwa miaka mitano ijayo.

Tume hiyo inakabiliwa pia na changamoto za kifedha, huku taarifa zilizowasilishwa bungeni zikionyesha kuwa ina upungufu wa takribani Sh11.02 bilioni katika bajeti inayohitajika kutekeleza shughuli zake na maandalizi ya uchaguzi.

Hivyo, suala la teknolojia ya uchaguzi linatarajiwa kuendelea kuzua mjadala kuhusu namna ya kuhakikisha uwazi na uwajibikaji bila kuongeza zaidi mzigo wa kifedha kwa walipa ushuru.