Watu watatu wamefariki dunia huku mmoja akinusurika baada ya boti waliyokuwa wakitumia kuvua samaki kugongwa na meli iliyokuwa ikisafiri kutoka Kisumu kuelekea Tanzania katika eneo la Kibuogi Beach, Kaunti ya Homa Bay.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Jumanne, Novemba 24, majira ya saa tatu usiku, katika eneo la Suba Kusini, na kusababisha hofu miongoni mwa wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Ziwa Victoria.

Waliofariki wametambuliwa kuwa Erick Ouma mwenye umri wa miaka 40, Joseph Ogolla mwenye miaka 38 na Pasaka Kanonge mwenye miaka 42.

Kwa mujibu wa naibu chifu wa eneo dogo la Sindo, Caroline Ngere, meli hiyo iliigonga boti ya wavuvi hao walipokuwa katika shughuli zao za uvuvi, na kusababisha wote kuanguka majini.

Ngere amesema wavuvi watatu walipotea baada ya ajali hiyo huku mmoja akiweza kujiokoa na kunusurika katika mkasa huo.

Amesema juhudi za kutafuta miili ya wavuvi hao zinaendelea, huku akitoa wito kwa vikosi vya kukabiliana na dharura na waokoaji kuharakisha operesheni hiyo ili miili hiyo ipatikane na kukabidhiwa kwa familia zao kwa ajili ya mazishi.

Tukio hilo limezua tena wasiwasi kuhusu usalama wa wavuvi wanaotumia vyombo vidogo vya majini kufanya shughuli zao katika Ziwa Victoria, hasa nyakati za usiku ambapo huenda ikawa vigumu kutambua vyombo vingine vinavyosafiri katika ziwa hilo.

Naibu chifu huyo amewataka wavuvi katika Ziwa Victoria kuhakikisha wanavaa makoti ya kujiokoa majini kila wanapoingia ziwani, akisisitiza kuwa vifaa hivyo ni muhimu katika kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za majini.

Ngere amebainisha kuwa huenda baadhi ya maisha yangeokolewa iwapo waathiriwa wa ajali hiyo wangekuwa wamevaa makoti hayo wakati wa tukio.

Aidha, amewahimiza wamiliki wa boti na wavuvi kuzingatia kanuni za usalama wanapotekeleza shughuli zao, ikiwemo kuhakikisha vyombo vyao vina vifaa vinavyohitajika kwa dharura.

Ziwa Victoria ni miongoni mwa maeneo muhimu ya shughuli za uvuvi nchini Kenya, likiendesha maisha ya maelfu ya familia katika kaunti za Homa Bay, Kisumu, Siaya na Migori.

Hata hivyo, ajali zinazohusisha boti za wavuvi na vyombo vikubwa vya majini zimeendelea kuibua changamoto kuhusu usalama wa usafiri na shughuli za kiuchumi katika ziwa hilo.

Familia za waliofariki sasa zinasubiri kupatikana kwa miili ya wapendwa wao huku shughuli za utafutaji zikiendelea.