Oburu Apendekeza Mfumo Wa Maridhiano Kuwateua Wagombea ODM 2027

Kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Dkt. Oburu Oginga, amependekeza mfumo wa maridhiano kutumika kuwateua wagombea watakaowania nyadhifa mbalimbali kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Oburu amewataka wanachama wa ODM kukumbatia mazungumzo na maridhiano katika kupata wagombea, akisema upigaji kura kupitia wajumbe wa chama utazingatiwa kama hatua ya mwisho iwapo maafikiano yatashindikana.

Hata hivyo, kiongozi huyo amesisitiza kuwa iwapo chama kitaamua kutumia mfumo wa kura ya siri kuwateua wagombea wake, uamuzi huo utaheshimiwa na kutekelezwa kama utaratibu rasmi wa chama.

Akizungumza katika makao makuu ya ODM, Chungwa House, wakati akipokea wanachama wapya waliojiunga na chama hicho, Oburu alitoa onyo kali kwa maafisa wa chama wanaodaiwa kupanga kupokea hongo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wanaowania tiketi ya ODM.

Alisema maafisa watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa lengo la kupendelea wagombea fulani watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu za chama.

Oburu amesisitiza kuwa chama hicho hakitavumilia vitendo vinavyoweza kuhujumu mchakato wa uteuzi wa wagombea, akiahidi kuwa zoezi hilo litafanyika kwa uwazi, haki na bila upendeleo.

Aidha, alisema uongozi wa ODM unaendelea kuziba mianya inayoweza kutumiwa na baadhi ya maafisa kuingilia mchakato wa uteuzi au kujinufaisha kifedha kutokana na azma ya wagombea kupata tiketi ya chama.
Kwa mujibu wa Oburu, maandalizi yanaendelea kuhakikisha kuwa mfumo wa uteuzi unaopangwa kufanyika Machi mwaka ujao unakuwa wa haki na unaowapa wagombea wote nafasi sawa ya kuwania tiketi za chama.

Katika kikao hicho, Oburu aliandamana na katibu mkuu wa chama Catherine Omanyo pamoja na mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, ambao waliunga mkono msimamo wake kuhusu umuhimu wa maridhiano na uchaguzi wa haki ndani ya chama.

Hatua hiyo inajiri huku vyama vya kisiasa vikianza kuweka mikakati ya ndani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, ambapo uteuzi wa wagombea unatarajiwa kuwa mojawapo ya hatua muhimu katika maandalizi ya uchaguzi huo.