Maafisa wa polisi nchini Colombia wamevamia duka kubwa la bidhaa za matumizi ya nyumbani (supermarket) na kuwaokoa watu 20 waliokuwa wakishikiliwa mateka kwa muda wa saa 17.

Operesheni hiyo ya uokoaji ilitekelezwa baada ya watu hao kunaswa ndani ya duka hilo katika mazingira yaliyosababisha wasiwasi kuhusu usalama wao.

Tukio hilo lilitokea katika duka la Éxito lililoko eneo la La Castellana, katika mji wa Cartagena, kaskazini mwa Colombia, baada ya washukiwa wenye silaha kuingia katika jengo hilo Jumanne asubuhi.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, washukiwa hao walikuwa wamejaribu kuteka gari la kubebea fedha na vitu vya thamani lililokuwa katika kituo hicho cha kibiashara lakini juhudi zao zikafeli, na hivyo kukimbilia ndani ya supermarket ambako waliwachukua watu waliokuwapo kama mateka.

Takriban watu 30 walikuwa wametekwa awali, wakiwemo wafanyakazi wa duka hilo na wateja. Hata hivyo, washukiwa hao waliwaachilia watu 10 wakati polisi wakiendelea na mazungumzo ya kutafuta suluhu ya amani.

Baada ya mazungumzo hayo kukosa mafanikio, vikosi maalum vya polisi na jeshi viliandaa operesheni ya kuwaokoa mateka waliokuwa wamesalia ndani ya jengo hilo.

Mashuhuda waliokuwa karibu na eneo hilo walisema walisikia milipuko kadhaa muda mfupi kabla ya maafisa wa usalama kuingia ndani ya supermarket. Polisi walithibitisha kutumia mabomu ya kutoa mshtuko (stun grenades) kuwazidi nguvu washukiwa hao.

Rais wa Colombia Abelardo de la Espriella alisema operesheni hiyo ilifanikiwa kuwaokoa mateka wote, huku mmoja wa watekaji akiuawa wakati wa makabiliano na vikosi vya usalama.

Alisema washukiwa hao walikuwa wamepewa nafasi ya kujisalimisha na kuwaachilia mateka lakini walikataa, hatua iliyosababisha mamlaka kuidhinisha operesheni ya kijeshi.

Rais huyo pia alikanusha madai kwamba tukio hilo lilihusisha makundi ya waasi au wanamgambo, akisema lilihusiana na wahalifu wa kawaida waliokuwa wamekwama baada ya jaribio lao la wizi kufeli.

Meya wa Cartagena alisema watu wote waliookolewa walikuwa salama na wangekutana na familia zao kabla ya kufanyiwa uchunguzi wa kiafya.

Wakati wa tukio hilo, helikopta ya polisi ilionekana ikizunguka eneo la supermarket huku maafisa wenye silaha nzito wakizingira jengo hilo.

Pia, shughuli za kutua kwa ndege katika uwanja wa ndege wa Rafael Núñez zilisitishwa kwa takriban dakika 45 kutokana na operesheni hiyo.

Tukio hilo limeibua wasiwasi kuhusu usalama nchini Colombia, wakati ambapo taifa hilo linaendelea kukabiliwa na mashambulizi ya makundi ya kihalifu na waasi licha ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa na waasi wa FARC mwaka 2023.