Gachagua Aikataa IEBC, Maraga Awasilisha Mapendekezo Ya Mageuzi
Muungano wa upinzani umetishia kuandaa maandamano kushinikiza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kushughulikia masuala yanayoibua utata kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Muungano huo unasema kuna masuala kadhaa yanayohitaji kushughulikiwa mapema ili kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.
Akizungumza na wanahabari Jumatano, aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga alisema muungano huo umependekeza marekebisho ya sheria za uchaguzi kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha IEBC inatekeleza majukumu yake bila kuingiliwa.
Maraga alisema mapendekezo hayo yanalenga kuipa tume uwezo na mifumo inayohitajika kusimamia uchaguzi unaozingatia matakwa ya Katiba.
Kwa upande wake, kinara wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, ametangaza kuwa upinzani hautashiriki mkutano wowote na IEBC kwa sasa, akidai kuwa uhuru na utendakazi wa tume hiyo umeathiriwa na ushawishi wa kisiasa.
Gachagua amemkosoa mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon, akimtuhumu kushindwa kushughulikia masuala muhimu yanayohusu maandalizi ya uchaguzi, yakiwemo kandarasi za ununuzi wa vifaa vya kielektroniki vya kusajili wapigakura na usafishaji wa sajili ya wapigakura.
Gachagua amesisitiza kuwa upinzani hautaendelea na mazungumzo ambayo hayajumuishi masuala waliyowasilisha kwa tume hiyo, akisema kufanya hivyo kutakuwa sawa na kupuuza hoja za Wakenya kuhusu uadilifu wa uchaguzi.
Mzozo huo unajiri wakati ambapo maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2027 yakizidi kushika kasi, huku upinzani ukitaka mageuzi ya kisheria na kiutendaji yafanyike mapema ili kuimarisha imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyowasilishwa na muungano huo ni kusafishwa kwa sajili ya wapigakura, kuondolewa kwa kituo cha kitaifa cha kujumlisha matokeo ya urais katika Bomas of Kenya, kuruhusu upigaji kura wa kielektroniki kwa Wakenya wanaoishi ughaibuni na kutangaza moja kwa moja shughuli za upigaji kura na kuhesabu kura.
Hata hivyo, utekelezaji wa mapendekezo hayo utategemea taratibu za kisheria na hatua zitakazochukuliwa na taasisi husika.
Hekaheka za upinzani za kupanga juu ya ninani apeperushe bendera kuelekea ikulu,zinaendelea.









