Mahakama imekataa ombi la kutaka kumzuia aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, kuendelea kuongoza chama cha National Economic Development Party (NEDP), hatua inayomruhusu kuendelea kutekeleza majukumu yake kama kiongozi wa chama hicho wakati mzozo wa uongozi ukiendelea.

Jaji wa Mahakama Kuu Roselyne Aburili alikataa ombi lililowasilishwa na wakili Nick Sanare, ambaye alikuwa akitaka amri za muda zitolewe kumzuia Sonko kuhudumu kama kiongozi wa chama hicho, mwanachama mwanzilishi au kushikilia nafasi yoyote katika uongozi wa NEDP.

Wakili Sanare anapinga ustahiki wa Sonko kuongoza chama hicho akitumia hoja kwamba aliondolewa madarakani kama Gavana wa Nairobi kupitia mchakato wa kumng'atua mamlakani (impeachment) mnamo Desemba 17, 2020.

Sanare anadai kuwa kuondolewa kwa Sonko madarakani kulithibitishwa na mahakama mbalimbali, ikiwemo Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu, hivyo kumfanya asistahili kushikilia nafasi za uongozi katika chama cha kisiasa.

Katika ombi lake, wakili huyo ametegemea Kifungu cha 75(3) cha Katiba pamoja na vifungu vya Sheria ya Vyama vya Kisiasa, akisema vinazuia watu walioondolewa madarakani kwa ukiukaji wa maadili kushikilia nyadhifa katika vyombo vya uongozi wa vyama.

Aidha, Sanare anaitaka mahakama kumzuia Msajili wa Vyama vya Kisiasa kumtambua au kumwandikisha Sonko kama mwanachama mwanzilishi au afisa wa NEDP.

Pia anataka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) izuiwe kupokea au kutumia vyeti vya uteuzi, orodha za wagombea au nyaraka nyingine zitakazotiwa saini na Sonko kwa niaba ya chama hicho.

Hata hivyo, mahakama ilielekeza kuwa kesi hiyo itatajwa tena Februari 3, 2027, kwa ajili ya kusikiliza hoja za pande husika na kupanga tarehe ya kutolewa kwa uamuzi.

Wakati huohuo, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imepinga kuendelea kushirikishwa katika kesi hiyo, ikisema mlalamikaji hajaonyesha hatua yoyote ya tume hiyo iliyokiuka wajibu wake wa kikatiba au kisheria.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa pia amepinga ombi la Sanare.

Uamuzi wa hivi punde unamaanisha kuwa Sonko ataendelea kutekeleza majukumu yake ndani ya NEDP kwa sasa, huku mahakama ikisubiri kuamua iwapo kikatiba anastahili kushikilia nafasi hiyo.