Kifo cha mwalimu mwenye umri wa miaka 23 kimezua ghadhabu katika Kaunti ya Homa Bay, huku walimu na wakazi wakitaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wahusika wa mauaji hayo ya kikatili.
George Owane, almaarufu Simba, aliuawa kwa kushambuliwa kwa mapanga siku 23 tu baada ya kuhitimu shahada ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Gretsa, na kuzima ndoto yake ya kuanza kazi ya ualimu.
Owane alihitimu Oktoba 30, 2026, baada ya kukamilisha masomo ya Shahada ya Elimu (Sanaa), akibobea katika Kiingereza na Fasihi.
Kwa mujibu wa taarifa za familia, siku ya Jumapili, Novemba 22, kijana huyo alitumia muda mwingi nyumbani na kaka yake kabla ya kuelekea katika kituo cha biashara cha Kadongo, eneo la Kabondo Kasipul, kufuatilia mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza kati ya Liverpool na Manchester United.
Hata hivyo, furaha ya kutazama soka iligeuka kuwa mkasa wakati wawili hao walipokuwa wakirejea nyumbani kwa miguu kuelekea kijiji cha Kanyamasawa.
Inadaiwa kuwa walikutana na wanaume wawili waliokuwa wamevalia makoti yanayofanana na sare za kijeshi, ambao waliwasimamisha na kuwauliza walikokuwa wakielekea.
Kaka yake Owane alisema awali walidhani watu hao walikuwa maafisa wa polisi waliokuwa wakifanya doria, kabla ya washambuliaji hao kuwavamia kwa mapanga.
Katika shambulizi hilo, Owane alipata majeraha mabaya yaliyosababisha kifo chake papo hapo, huku kaka yake akijeruhiwa sikioni na kunusurika.
Baba yake, Blastus Owane, ambaye pia ni mwalimu, alisema familia ilikuwa na matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa mwanawe baada ya kuhitimu, lakini matumaini hayo yamekatizwa na mauaji hayo.
Familia sasa inataka uchunguzi wa haraka kufanywa na wote waliohusika kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
Mauaji hayo pia yameibua wasiwasi kuhusu usalama katika eneo hilo, huku waendesha bodaboda wakiandamana hadi Kituo cha Polisi cha Othoro kudai hatua madhubuti dhidi ya ongezeko la visa vya uhalifu.
Kamanda wa Polisi wa Rachuonyo Mashariki, Sheila Kegode, alisema polisi wameanzisha uchunguzi na wanafuatilia vidokezo kadhaa ili kuwakamata washukiwa.
Aliwataka wakazi kutoa taarifa zitakazosaidia uchunguzi, akihakikishia umma kuwa polisi watahakikisha waliohusika wanakabiliwa na sheria.
Mbunge wa Kabondo Kasipul, Eve Obara, pia amelaani mauaji hayo, akisema hakuna tofauti inayopaswa kuwa sababu ya mtu kupoteza maisha.









