Watu watano wameuawa na wengine wanne kujeruhiwa kufuatia uvamizi wa kutumia silaha uliotekelezwa Jumapili jioni katika Kijiji cha Elsa Ntirim, Wadi ya Burat, Kaunti ya Isiolo, huku hofu ikitanda miongoni mwa wakazi kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama katika eneo hilo.
Washambuliaji walivamia kijiji hicho na kuua watu watano katika tukio lililozua taharuki, huku majeruhi wakikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Isiolo kwa matibabu ya dharura.
Tukio hilo limetokea siku moja tu baada ya Kamati ya Usalama ya Bunge la Kitaifa kufanya mkutano katika eneo hilo kwa lengo la kutafuta suluhu ya migogoro ya muda mrefu inayohusisha wizi wa mifugo na mauaji ya kiholela.
Miongoni mwa waliojeruhiwa ni James Waweru na William Kinyore, ambao wanaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Isiolo.
Afisa Mkuu wa Idara ya Afya katika Kaunti ya Isiolo, Mohamud Abdikadir, amesema majeruhi hao wanahitaji msaada wa haraka wa damu ili kuwawezesha kupata matibabu zaidi.
Abdikadir amefichua kuwa hali ya mmoja wa majeruhi ilihitaji uangalizi wa kiwango cha juu zaidi, hali iliyosababisha kusafirishwa hadi Kaunti ya Meru kwa matibabu maalumu.
Wakati huohuo, Naibu Gavana wa Isiolo, Dkt. James Lowasa, ameelezea masikitiko yake kuhusu kuendelea kuzorota kwa usalama katika eneo hilo licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na viongozi wa serikali kutafuta suluhu ya migogoro hiyo.
Lowasa ameitaka serikali na vyombo vya usalama kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu mazingira ya uvamizi huo, akipendekeza pia kuchunguzwa kwa madai yanayohusisha baadhi ya washambuliaji na hifadhi za wanyamapori zinazosimamiwa na jamii.
Amesema madai hayo yanahitaji kuchunguzwa ili kubaini ukweli na kuhakikisha wahusika wowote wanaohusika na machafuko wanachukuliwa hatua za kisheria.
Uvamizi huo umeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa wakazi wa Isiolo, eneo ambalo limekuwa likikumbwa na migogoro inayohusishwa na wizi wa mifugo, mashambulizi ya kulipiza kisasi na mauaji.
Wakazi wameendelea kukabiliwa na hofu ya mashambulizi mapya huku familia zikihangaika kutokana na vifo na majeraha yaliyotokana na tukio hilo.
Hata hivyo, tukio hilo sasa linaweka shinikizo zaidi kwa viongozi wa serikali ya kitaifa na kaunti kuhakikisha hatua madhubuti zinachukuliwa kurejesha usalama, kuwakamata washukiwa na kuzuia umwagikaji zaidi wa damu katika eneo hilo.









