Zaidi ya walimu wakuu 15,000 kutoka shule mbalimbali nchini wamekusanyika jijini Mombasa kwa mkutano wa siku nne unaolenga kujadili mustakabali wa sekta ya elimu, mageuzi ya mitaala na changamoto zinazokabili utekelezaji wa mfumo mpya wa elimu nchini.
Mkutano huo ulioandaliwa na Chama cha Wakuu wa Shule za Comprehensive (KECSHA), unafanyika kuanzia Novemba 9 hadi 12, 2026, katika kituo cha Sheikh Zayed Children Welfare Centre, huku ukitarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa elimu kujadili namna ya kuboresha utoaji wa elimu nchini.
Ajenda kuu katika mkutano huo ni pamoja na utekelezaji wa mabadiliko ya mitaala, kuimarisha uongozi wa shule, kuboresha viwango vya ufundishaji na kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na ujuzi unaohitajika katika dunia inayobadilika kwa kasi.
Mwenyekiti wa kitaifa wa KECSHA, Fuad Ali, amesema mkutano huo unatoa nafasi kwa viongozi wa shule kutathmini namna taasisi za elimu zinavyopaswa kukabiliana na mahitaji mapya ya wanafunzi, maendeleo ya teknolojia na matarajio yanayoongezeka kuhusu uwajibikaji katika sekta hiyo.
Miongoni mwa masuala yanayotarajiwa kujadiliwa ni changamoto za utekelezaji wa mfumo wa elimu, usimamizi wa shule za msingi na Junior School, pamoja na masuala ya kitaaluma na kiutawala yanayohusu walimu na Tume ya Huduma za Walimu (TSC).
Pia, mkutano huo unatarajiwa kuangazia pengo linaloendelea kujitokeza katika ujuzi wa msingi wa kusoma, kuandika na kuhesabu miongoni mwa wanafunzi wa madarasa ya chini.
Utafiti uliofanywa na CEMASTEA kwa kushirikiana na taasisi ya Echidna katika kaunti 15 ulionyesha kuwa ni asilimia 10.1 pekee ya walimu wanaofundisha watoto wa PP1 na PP2 waliofikia kiwango kilichowekwa cha umahiri wa ufundishaji wa hesabu.
Kwa walimu wanaofundisha Gredi ya Kwanza hadi ya Tatu, ni takriban asilimia 40 pekee waliofikia kiwango hicho, hali inayoibua wasiwasi kuhusu msingi wa maarifa yanayopaswa kujengwa katika miaka ya mwanzo ya masomo.
Mbali na mijadala, washiriki watapata mafunzo maalumu kuhusu matumizi ya teknolojia katika elimu, ushirikishwaji wa wazazi, usimamizi wa fedha za shule, afya ya wanafunzi na mbinu bora za uongozi.
Rais William Ruto anatarajiwa kuhudhuria hafla ya kufunga mkutano huo, ambapo wasimamizi wa shule watapata fursa ya kuwasilisha changamoto zao na mapendekezo kuhusu sera za elimu.
Mkutano huo unafanyika wakati sekta ya elimu nchini ikiendelea kupitia mabadiliko makubwa yanayohitaji ushirikiano wa serikali, walimu, wazazi na wadau wengine ili kuhakikisha mageuzi hayo yanaleta matokeo yanayotarajiwa.









