Jeshi la Sudan limewakamata tena Ahmed Haroun, aliyekuwa kiongozi wa chama tawala cha National Congress Party (NCP) wakati wa utawala wa aliyekuwa Rais Omar al-Bashir, ambaye anatafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusiana na tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika eneo la Darfur.

Haroun, ambaye pia alikuwa mmoja wa maafisa wakuu wa serikali ya Bashir, alitiwa mbaroni Jumapili Novemba 8, 2026, huku maafisa wawili wa chama chake wakithibitisha kukamatwa kwake.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na maafisa wa usalama, Haroun alichukuliwa chini ya ulinzi kwa kufuata taratibu za kisheria, ingawa sababu kamili za kukamatwa kwake hazijawekwa wazi.

Kukamatwa kwake kunajiri siku chache baada ya kuibuka tena hadharani kupitia mahojiano ya takriban saa nne katika kipindi cha mazungumzo ya Sudan Podcast, ambapo alizungumzia masuala mbalimbali kuhusu siasa za nchi hiyo na vita vinavyoendelea kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF).

Katika mahojiano hayo, Haroun alisema chama chake na jeshi huenda visiwe na misimamo sawa kisiasa, lakini vinaunganishwa na vita dhidi ya RSF.

Hatua hiyo imezua maswali kuhusu sababu zilizofanya jeshi kumkamata mtu ambaye amekuwa akihusishwa na harakati zinazounga mkono operesheni zake dhidi ya RSF.

Haroun alikamatwa kwa mara ya kwanza Aprili 2019 kufuatia kuondolewa madarakani kwa Bashir baada ya maandamano makubwa ya wananchi yaliyodumu kwa miezi kadhaa.

Hata hivyo, mwaka 2023, alitoroka gerezani pamoja na maafisa wengine wa serikali ya zamani wakati vita vilipozuka kati ya jeshi la Sudan na RSF.

ICC imekuwa ikimtaka Haroun akabidhiwe ili kukabili mashtaka yanayohusiana na matukio ya umwagaji damu katika eneo la Darfur mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Anakabiliwa na makosa 20 ya uhalifu dhidi ya binadamu na mashtaka 22 ya uhalifu wa kivita, yanayohusishwa na madai ya kushiriki katika kuandikisha wapiganaji wa kundi la Janjaweed, lililotuhumiwa kutekeleza mauaji ya kikabila, ubakaji na mashambulizi dhidi ya raia.

Haroun amekuwa akipinga tuhuma hizo akizitaja kuwa za kisiasa.

Wakati huo huo, Sudan imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili 2023, baada ya mvutano kati ya jeshi linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan na RSF kugeuka kuwa mapigano makali.

Vita hivyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, njaa na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao, huku Umoja wa Mataifa ukivitaja kuwa miongoni mwa majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani.

Hadi sasa, jeshi la Sudan na ICC hazijatoa maelezo rasmi kuhusu hatua zinazofuata dhidi ya Haroun.