Umoja wa Mataifa umetenga zaidi ya Sh387 milioni kusaidia maelfu ya raia wa Ethiopia waliokimbilia nchini Kenya kutafuta hifadhi kufuatia mapigano ya kikabila yanayoendelea katika maeneo ya kusini mwa Ethiopia, karibu na mpaka wa nchi hizo mbili.

Fedha hizo, zinazokadiriwa kuwa dola milioni tatu za Marekani, zitatumika kutoa msaada wa dharura kwa takriban watu 50,000 waliovuka mpaka na kuingia katika eneo la Moyale, Kaunti ya Marsabit.

Mratibu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya dharura za kibinadamu, Tom Fletcher, alitangaza mgao huo Novemba 6, akisema fedha hizo zitatolewa kupitia Hazina Kuu ya Umoja wa Mataifa ya Kukabiliana na Dharura (CERF).

Msaada huo unalenga kuhakikisha familia zilizoathiriwa zinapata mahitaji muhimu yakiwemo chakula, maji safi na salama, makazi ya muda pamoja na huduma za afya.

Idadi ya watu wanaovuka mpaka imeendelea kuongezeka tangu mapigano yalipozuka katika eneo la Moyale nchini Ethiopia, huku wanawake na watoto wakitajwa kuwa sehemu kubwa ya wanaotafuta hifadhi nchini Kenya.

Baadhi ya wakimbizi hao wamepata hifadhi katika shule, majengo ya umma na maeneo ya wazi, huku wengine wakipokelewa na familia katika jamii zinazopakana na Ethiopia.

Hata hivyo, ongezeko hilo limeanza kuweka shinikizo kubwa kwa huduma muhimu katika eneo la Moyale, hasa upatikanaji wa maji, vyoo, chakula na huduma za matibabu.

Ripoti za mashirika ya kibinadamu zinaonyesha kuwa baadhi ya maeneo yanayohifadhi wakimbizi yanakabiliwa na upungufu wa vyoo, vifaa vya kunawia mikono na mifumo ya kuhifadhi maji.

Hatua ya Umoja wa Mataifa inajiri siku chache baada ya mashirika ya UNHCR, UNICEF, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kutoa ombi la kutafuta takriban Sh1.16 bilioni ili kusaidia watu 50,000 kwa kipindi cha miezi mitatu.

Wakati huohuo, hali ya usalama katika mpaka wa Kenya na Ethiopia imeendelea kuwa ya wasiwasi kutokana na uwezekano wa mapigano kuvuka na kuathiri maeneo ya Kenya.

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja ametangaza kuimarishwa kwa doria na ufuatiliaji wa usalama katika eneo hilo ili kuwalinda wakazi na mali zao.

Mapigano hayo yanayohusisha vikosi vinavyohusishwa na maeneo ya Oromia na Somali nchini Ethiopia yamesababisha maelfu ya familia kuyahama makazi yao, huku mashirika ya kibinadamu yakionya kuwa mahitaji yanaweza kuongezeka iwapo hali ya usalama haitaimarika.