Marekani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zimeimarisha ushirikiano wao wa kiuchumi na kimkakati kupitia mazungumzo yaliyofanyika jijini Paris, Ufaransa, yakilenga kuongeza uwekezaji, kuimarisha usalama na kukuza biashara kati ya mataifa hayo mawili.

Wawakilishi wa serikali hizo walikutana kwa mara ya pili katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya Uongozi (JSC), kinachosimamia utekelezaji wa Mkataba wa Ushirikiano wa Kimkakati kati ya Marekani na DRC.

Katika mkutano huo, pande zote mbili zilithibitisha dhamira yao ya kushirikiana katika kukuza uchumi, kuimarisha utulivu na kuongeza ustawi wa wananchi wa mataifa hayo.

Kamati hiyo ina jukumu la kuelekeza utekelezaji wa makubaliano hayo na kuhakikisha ahadi zilizotolewa zinabadilishwa kuwa miradi halisi yenye majukumu yaliyo wazi, muda maalumu wa utekelezaji na matokeo yanayoweza kupimwa.

Katika mkutano huo, wajumbe walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya wizara, mashirika ya serikali na taasisi za kiufundi za nchi zote mbili ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi.

Aidha, walipitia maendeleo yaliyopatikana tangu mkutano wao wa kwanza uliofanyika Februari 2026, huku wakikaribisha kuongezeka kwa hamu ya kampuni za Marekani kuwekeza katika mpango wa Hifadhi ya Mali za Kimkakati (Strategic Asset Reserve).

Shirika la Marekani la Ufadhili wa Maendeleo ya Kimataifa (DFC) pia liliwasilisha taarifa kuhusu ongezeko la miradi ya uwekezaji inayochunguzwa na kuandaliwa kwa ajili ya kutekelezwa nchini DRC.

Miongoni mwa hatua muhimu zilizojadiliwa ni kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano ya uendeshaji wa Ukanda wa Lobito (Lobito Corridor), unaotarajiwa kuimarisha biashara na usafirishaji wa bidhaa katika ukanda huo wa Afrika.

Viongozi hao pia walijadili hatua zinazofuata katika mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Grand Inga, pamoja na fursa za uchakataji na usafirishaji wa madini muhimu na uwekezaji katika sekta ya nishati.

Marekani na DRC pia zilitambua kupitishwa kwa sheria mpya nchini Congo inayoweka masharti ya kodi na ushuru wa forodha kwa miradi inayotekelezwa chini ya mkataba huo.

Katika makubaliano hayo, pande zote zilisisitiza kuwa wananchi wa Congo wanapaswa kunufaika na utajiri wa rasilimali za nchi yao kupitia ajira, mafunzo ya ujuzi na ukuaji wa kampuni za ndani pamoja na zile za Marekani.

Aidha, zilieleza kuwa amani na usalama ni msingi muhimu wa utekelezaji wa makubaliano hayo na ustawi wa muda mrefu wa DRC.

Mataifa hayo yamesisitiza dhamira ya kubadilisha makubaliano yao kuwa uwekezaji wa kudumu utakaotengeneza ajira, kuimarisha minyororo ya usambazaji bidhaa na kukuza uchumi wa wananchi wa nchi zote mbili.