Katika kuendana na mikakati ya serikali ya kuimarisha utendaji wa taasisi za umma, Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ametangaza uteuzi wa watu 13 kwa nyadhifa mbalimbali katika wizara, idara na taasisi za serikali.
Uteuzi huo unahusisha nafasi za makatibu wakuu wa wizara mbalimbali pamoja na nyadhifa nyingine muhimu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tume ya Utumishi wa Umma na Bunge la Uganda.
Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, Museveni alisema amefanya uteuzi huo kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Ibara ya 174(2) ya Katiba ya Uganda ya mwaka 1995.
Hata hivyo, rais huyo ameiagiza Tume ya Utumishi wa Umma kuchunguza uwezo na kufaa kwa watu waliopendekezwa kushikilia nyadhifa hizo kabla ya kumpa ushauri kuhusu kukamilisha uteuzi wao.
Miongoni mwa waliopendekezwa ni Emmanuel Freddie Mugunga, atakayehudumu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Maureen Kasande katika Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali na Sheeba Kyobutungi Rujoki katika Ofisi ya Rais inayoshughulikia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.
Wengine ni Kenneth Akiri katika Wizara ya Maji na Mazingira, Barbara Namugambe katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, pamoja na Charles Ssentongo katika Wizara ya Mambo ya Nje.
Profesa Stephen Akandwanaho amependekezwa kuongoza Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Mwongozo wa Kitaifa, huku Mark Sseremba akipendekezwa katika Wizara ya Utumishi wa Umma.
Katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Flavia Guto Bwire ndiye aliyependekezwa, huku Edith Butuuro akitajwa kwa Wizara ya Ulinzi na Masuala ya Wastaafu wa Kijeshi.
Aidha, Aggrey Wunyi amependekezwa katika Wizara ya Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku Betty Mutesa Cwinya-ai akitajwa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma.
Mteule mwingine ni Dkt. Edward Sengonzi Damulira, aliyependekezwa kuwa Karani wa Bunge la Uganda, akichukua nafasi ya Adolf Mwesigye.
Mabadiliko hayo yanagusa taasisi zinazohusika na usimamizi wa shughuli za serikali, utekelezaji wa sera, usalama, diplomasia, miundombinu na ushirikiano wa kikanda.
Kwa mujibu wa maelekezo ya Museveni, hatua inayofuata ni Tume ya Utumishi wa Umma kufanya tathmini ya waliopendekezwa na kuwasilisha ushauri wake kwa rais kabla ya mchakato wa uteuzi kukamilishwa.









