Uchunguzi wa miili na utambuzi rasmi wa watu wanane waliofariki dunia kufuatia kuporomoka kwa jengo la ghorofa 18 katika eneo la Eastleigh jijini Nairobi unaendelea katika hifadhi ya maiti ya Nairobi Funeral Home.
Uchunguzi huo wa kitaalamu unalenga kubaini chanzo cha vifo vya wahanga hao pamoja na kuwezesha utambuzi wa miili yao kupitia vipimo vya vinasaba (DNA), hatua itakayosaidia familia kupata uhakika kuhusu ndugu zao na kuanza maandalizi ya mazishi.
Miili hiyo inajumuisha wanawake sita na wanaume wawili waliokuwa miongoni mwa watu waliokuwa wamekwama chini ya vifusi vya jengo hilo lililoporomoka Oktoba 23, kando ya Barabara ya 9th Street, Eastleigh.
Kuporomoka kwa jengo hilo kulizua operesheni kubwa ya uokoaji iliyohusisha vikosi mbalimbali vya usalama, wahudumu wa dharura na wataalamu wa uokoaji waliotumia mitambo mizito kuondoa vifusi na kutafuta watu waliokuwa wamefunikwa na zege.
Watu wanne waliokolewa wakiwa hai, huku wengine watatu ambao awali waliripotiwa kutoweka wakiendelea kutafutwa na familia zao licha ya kukamilika kwa operesheni ya siku 15 ya uokoaji na urejeshaji wa miili.
Serikali ya Kaunti ya Nairobi imeahidi kusaidia familia zilizoathiriwa kugharamia vipimo vya DNA, huduma za hifadhi ya maiti pamoja na mipango ya mazishi.
Kuhusu jengo lenyewe...
Jengo hilo la ghorofa 18 lilikuwa bado katika hatua za ujenzi wakati wa mkasa huo, huku baadhi ya shughuli za kibiashara zikiendelea katika sehemu za chini za jengo hilo.
Taarifa zilizotolewa baada ya mkasa huo zilionyesha kuwa mradi huo ulikuwa umezungukwa na maswali kuhusu uidhinishaji wa ujenzi na uzingatiaji wa kanuni za usalama.
Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alifichua kuwa michoro ya usanifu iliyowasilishwa kwa serikali ya kaunti Novemba 2024 haikuwa imeidhinishwa, licha ya ujenzi kuendelea.
Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) ilisema mradi huo ulisajiliwa Julai 30, 2025, lakini usajili huo haukumaanisha kuwa vibali vyote muhimu vya ujenzi vilikuwa vimepatikana.
Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) pia ilisema mradi huo haukuwa na leseni ya tathmini ya athari za kimazingira.
Maafa hayo yameibua upya maswali kuhusu usimamizi wa ujenzi wa majengo marefu jijini Nairobi, uwajibikaji wa wakandarasi na uwezo wa mamlaka husika kuhakikisha kanuni za usalama zinafuatwa kabla ya majengo kutumiwa na umma.









