Wafanyabiashara Sori Walia Hasara Baada Ya Moto Kuteketeza Soko
Wafanyabiashara katika Soko la Sori, eneo bunge la Nyatike, wameachwa katika hali ya sintofahamu baada ya moto kuzuka na kuteketeza biashara zao usiku wa kuamkia leo, katika tukio linaloshukiwa kusababishwa na hitilafu ya mfumo wa umeme.
Tukio hilo limewaacha wafanyabiashara wengi katika hali ngumu, huku baadhi yao wakihofia kupoteza chanzo chao kikuu cha mapato kutokana na uharibifu uliosababishwa na moto huo.
Katika ujumbe wa kuwapa pole wafanyabiashara walioathirika, kiongozi wa eneo hilo alieleza masikitiko yake kuhusu mkasa huo, akisema kuwa biashara nyingi zilizoteketea zilikuwa tegemeo pekee la kifedha kwa familia za wamiliki wake.
Alisema kuwa wafanyabiashara hao, ambao wamekuwa wakijituma kila siku kutafuta riziki, sasa wanakabiliwa na changamoto ya kuanza upya baada ya kupoteza bidhaa na mali zao katika mkasa huo.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa jamii kuungana na kuwasaidia waathiriwa kurejesha shughuli zao za kiuchumi badala ya kuwaacha wakabiliane na athari za mkasa huo pekee yao.
Alifichua kuwa timu yake tayari imefika katika eneo la tukio ili kutathmini kiwango cha uharibifu na kubaini mahitaji ya dharura yanayohitaji kushughulikiwa ili kuwasaidia wafanyabiashara kurejelea shughuli zao.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa waathiriwa wanapata msaada unaohitajika katika kipindi hiki kigumu, huku akitoa wito kwa wakazi na wadau mbalimbali kujitokeza kuonyesha mshikamano.
Moto huo unatarajiwa kuibua upya mjadala kuhusu usalama wa mifumo ya umeme katika masoko ya umma, pamoja na umuhimu wa kuwepo kwa mikakati madhubuti ya kuzuia na kukabiliana na majanga ya moto.
Hata hivyo, chanzo halisi cha moto huo bado hakijathibitishwa rasmi, huku tathmini ya hasara ikitarajiwa kubainisha ukubwa wa mali zilizoharibiwa.
Wafanyabiashara walioathirika sasa wanakabiliwa na jukumu la kujenga upya biashara zao na kurejesha maisha yao ya kila siku.
Visa vya moto vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara nchini,huku kukiwa na madai ya wahuskia kukosa elimu ya msingi kuhusina na namna ya kukabiliana na majanga ya dharura kwa wakati.









