Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dk. Patrice Motsepe, amefafanua sababu za kurejesha mfumo wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kufanyika kila baada ya miaka miwili, akisema hatua hiyo inalenga kulinda maslahi ya soka la Afrika.

Motsepe amesema Kamati ya Utendaji ya CAF (EXCO) ilizingatia maslahi ya vyama 54 wanachama wa shirikisho hilo pamoja na wachezaji wa Afrika wanaocheza katika klabu mbalimbali nje ya bara hilo kabla ya kufikia uamuzi huo.

Ameeleza kuwa mpango wa awali wa kuanzisha mashindano mapya yaliyopewa jina la Africa Nations League, yaliyopendekezwa kuchukua nafasi ya AFCON na kufanyika kila baada ya miaka miwili, ungehitaji muda mrefu kabla ya kuanza kutoa manufaa makubwa ya kifedha na kuchangia maendeleo ya soka barani Afrika.

Kwa mujibu wa Motsepe, kuendeleza AFCON katika mfumo wake wa sasa kutasaidia kulinda thamani ya mashindano hayo na kuhakikisha vyama wanachama vinaendelea kunufaika na mapato yanayotokana na michuano hiyo.

Amesema AFCON ijayo itafanyika mwaka 2027 katika mataifa matatu ya Afrika Mashariki, Kenya, Tanzania na Uganda, akieleza matumaini yake kuwa mashindano hayo yataandaliwa kwa mafanikio.

Baada ya toleo hilo, mashindano mengine ya AFCON yanatarajiwa kufanyika mwaka 2028, 2031 na 2033.

Motsepe amefafanua kuwa hakutakuwa na fainali za AFCON mwaka 2030 kutokana na kufanyika kwa Kombe la Dunia la FIFA, kwa kuzingatia kalenda ya kimataifa ya soka.

AFCON ni mojawapo ya mashindano makubwa na yenye historia ndefu zaidi katika soka la Afrika. Toleo la kwanza lilifanyika mwaka 1957 nchini Sudan, likishirikisha mataifa matatu pekee yaliyokuwa Misri, Sudan na Ethiopia, baada ya Afrika Kusini kutoshiriki.

Misri ilitwaa ubingwa wa kwanza na baadaye kujijengea rekodi ya mafanikio katika mashindano hayo. Kwa miaka mingi, AFCON imekua na kuwa jukwaa muhimu la kuonyesha vipaji vya wachezaji wa Afrika na kuimarisha ushindani wa soka la mataifa.

Katika miaka ya hivi karibuni, mashindano hayo yameendelea kuvutia mashabiki wengi duniani, huku yakitoa fursa kwa nchi mwenyeji kukuza utalii na uchumi kupitia wageni, wadhamini na shughuli za kibiashara.

Motsepe amesisitiza kuwa AFCON si mashindano ya soka pekee, bali pia ni jukwaa la kuadhimisha utamaduni, mila na desturi za Afrika, huku likiunganisha watu kutoka mataifa 54 ya bara hilo, diaspora ya Afrika na sehemu nyingine duniani.

Amesema uamuzi wa kuendeleza mashindano hayo kila baada ya miaka miwili unalenga kuhakikisha soka la Afrika linaendelea kukua na kuwa na ushindani mkubwa kimataifa.