Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, ameendelea kuvutia hisia za watu duniani kutokana na maisha yake ya ndoa, baada ya kuingia madarakani akiwa na wake wawili, hali inayomfanya kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo kushika wadhifa wa urais akiwa katika ndoa ya wake wengi.

Faye, aliyechaguliwa kuwa rais wa Senegal mwaka 2024, ameoa wanawake wawili ambao wamekuwa sehemu ya maisha yake ya kifamilia na safari yake ya kisiasa hadi kuingia Ikulu.

Mke wake wa kwanza ni Marie Khone Faye, ambaye alifunga naye ndoa mwaka 2009.

Marie anatoka kijiji cha Ndiaganiao, eneo ambalo pia ndilo alikozaliwa rais huyo.

Wawili hao wamebarikiwa kupata watoto wanne, wavulana watatu na msichana mmoja, katika kipindi cha miaka kadhaa ya ndoa yao.

Kwa upande mwingine, Faye alifunga ndoa na mke wake wa pili, Absa Faye, mwaka 2023, takribani mwaka mmoja kabla ya kushinda uchaguzi wa urais.

Maisha ya ndoa ya rais huyo yaliibuka kuwa gumzo kimataifa wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais wa mwaka 2024, baada ya kuamua kujitokeza hadharani akiwa ameshikana mikono na wake zake wote wawili.

Tukio hilo lilizua mijadala mikubwa nchini Senegal na nje ya mipaka yake, huku picha za familia hiyo zikisambaa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Kwa wengi, hatua ya Faye kuwatambulisha wake zake wawili mbele ya umma ni ishara ya uwazi kuhusu maisha yake binafsi, hasa katika jamii ambako ndoa za wake wengi zina nafasi katika mila na baadhi ya desturi za kidini.

Senegal ni miongoni mwa mataifa ya Afrika Magharibi ambako ndoa za wake wengi zimekuwepo kwa muda mrefu, ingawa utamaduni huo pia umekuwa ukizua mijadala kuhusu haki za wanawake na usawa ndani ya familia.

Mwanasosholojia Djiby Diakhaté aliwahi kueleza kuwa kujitokeza kwa Faye akiwa na wake zake wawili kulionyesha uhalisia wa baadhi ya familia nchini humo, ambako mfumo huo wa ndoa umekita mizizi.

Hata hivyo, suala hilo limepokea mitazamo tofauti, huku baadhi ya wanawake wakieleza wasiwasi kuhusu changamoto zinazoweza kujitokeza katika ndoa za wake wengi.

Faye aliapishwa kuwa rais wa tano wa Senegal Aprili 2, 2024, baada ya kushinda uchaguzi wa Machi 24, akipata asilimia 54.28 ya kura.

Tangu wakati huo, maisha yake ya kifamilia yameendelea kuwa miongoni mwa mambo yanayomfanya kuvutia umakini wa umma, huku wake zake wawili wakitambulika kama sehemu ya familia ya kwanza ya Senegal.

Afrika,marais wengi wametajwa kuwa na wanawake zaidi ya mmoja akiwemo Omar El Bashir,Jomo Kenyatta,Jacob Zuma na wengine.

Ingawa hawa hawakuteza kuwaonyesha wake hao mbele ya umma.