Sekta ya filamu duniani imepoteza mmoja wa waigizaji mahiri zaidi, Sir Patrick Stewart, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 86, akiacha urithi mkubwa kupitia majukumu yaliyogusa mamilioni ya mashabiki duniani.

Stewart, aliyefahamika zaidi kwa kuigiza Profesa Charles Xavier katika filamu za X-Men, alifariki Oktoba 28, 2026, nyumbani kwake Los Angeles, Marekani, baada ya kukabiliana na maradhi ya Alzheimer na Lewy body dementia.

Safari yake ya mafanikio ni simulizi ya mtu aliyetoka katika familia yenye maisha magumu na kujijengea jina kubwa kupitia kipaji, bidii na kujitolea katika sanaa ya uigizaji.

Alizaliwa Julai 13, 1940, katika mji wa Mirfield, Yorkshire, Uingereza. Stewart alikulia katika familia ya kipato cha chini, huku changamoto za kifamilia zikifanya maisha yake ya utotoni kuwa magumu.

Hata hivyo, mapenzi yake kwa uigizaji yalianza akiwa shuleni, ambako mwalimu wake alimtia moyo kujifunza na kuigiza kazi za mwandishi maarufu William Shakespeare.

Akiwa na umri wa miaka 15, aliacha shule na kuelekeza nguvu zake katika uigizaji, hatua iliyoweka msingi wa safari yake iliyodumu zaidi ya miongo sita.

Umaarufu wake wa kimataifa uliongezeka alipoigiza Kapteni Jean-Luc Picard katika mfululizo wa Star Trek: The Next Generation, kabla ya kupata nafasi ya Profesa Charles Xavier katika filamu ya X-Men ya mwaka 2000.

Katika filamu hizo, alicheza kiongozi mwenye hekima na uwezo wa kipekee wa kiakili, aliyekuwa akiongoza kundi la mutants kupigania amani na kukabiliana na ubaguzi.

Miongoni mwa filamu nyingine alizoshiriki ni X2: X-Men United (2003), X-Men: The Last Stand (2006), X-Men: Days of Future Past (2014), Logan (2017) na Doctor Strange in the Multiverse of Madness (2022).

Pia alionyesha uwezo wake katika filamu za Dune (1984), Conspiracy Theory (1997) na The Prince of Egypt (1998), akithibitisha uwezo wake wa kucheza wahusika wa aina mbalimbali.

Mchango wake katika sanaa ulitambuliwa mwaka 2010 alipotunukiwa heshima ya uungwana na Malkia Elizabeth II kutokana na mchango wake katika maigizo.

Kifo chake kinaacha pengo kubwa katika tasnia ya burudani, huku mashabiki wakikumbuka kipaji chake, sauti yake ya kipekee na wahusika aliowapa uhai kwenye skrini.

Patrick Stewart, 1940–2026,gwiji aliyeondoka, lakini kazi zake zitaendelea kuishi katika mioyo ya mashabiki.