Saudi Arabia imesitisha utoaji wa visa za aina zote kwa wasafiri wanaotoka Kenya na kupiga marufuku kuingia nchini humo kwa watu wanaowasili kutoka Kenya kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea kushughulikiwa nchini.

Hatua hiyo imetangazwa Ijumaa, Oktoba 30, 2026, na Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA), kufuatia tathmini ya hali ya maambukizi iliyofanywa na mamlaka za afya nchini humo.

Kupitia hatua hizo za tahadhari, Saudi Arabia pia imesitisha safari za raia wake kuelekea Kenya ili kupunguza uwezekano wa kuenea kwa virusi vya Ebola katika Ufalme huo.

Marufuku hiyo inawahusu pia wasafiri wanaotaka kuingia Saudi Arabia kupitia mataifa mengine, iwapo watakuwa wameishi au kukaa Kenya au nchi nyingine zinazokabiliwa na mlipuko wa Ebola ndani ya siku 21 kabla ya kuwasili kwao.

Mamlaka za Saudi Arabia zimesema uamuzi huo ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha usalama wa afya ya umma na kuzuia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza kuvuka mipaka.

Hata hivyo, Mamlaka ya Afya ya Umma nchini Saudi Arabia, Weqaya, imewahakikishia wananchi kuwa hali ya afya nchini humo inaendelea kuwa shwari, huku ufuatiliaji wa karibu ukiendelea kwa kushirikiana na taasisi za afya za ndani na kimataifa.

Hatua hiyo mpya inakuja wakati Kenya ikiendelea kukabiliana na mlipuko wa Ebola wa aina ya Bundibugyo, ambao kufikia Oktoba 30 ulikuwa umethibitisha maambukizi tisa na kusababisha vifo vya watu wawili.

Wizara ya Afya imesema Kenya ilikuwa imekamilisha siku 10 bila kuripoti maambukizi mapya, kufuatia hatua za kudhibiti mlipuko huo na kufuatilia watu waliokuwa wamekutana na wagonjwa.

Katibu Mkuu wa Afya ya Umma, Mary Muthoni, alisema watu waliokuwa chini ya uangalizi wa lazima wa siku 21 wanaachiliwa kwa awamu baada ya kukamilisha kipindi hicho bila kuonyesha dalili za ugonjwa.

Watu 20 wa kwanza walikamilisha ufuatiliaji huo Oktoba 26, huku wengine 46 wakitarajiwa kuachiliwa Novemba 3.

Saudi Arabia tayari ilikuwa imechukua hatua kama hizo mwezi Juni mwaka huu dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Uganda na Sudan Kusini kutokana na hatari ya Ebola.

Hatua hizo zinaongeza changamoto kwa Wakenya wanaopanga kusafiri Saudi Arabia kwa shughuli za kikazi, kibiashara na ziara nyingine, huku kukiwa na haja ya kufuatilia matangazo rasmi kuhusu masharti mapya ya safari.