Rais wa Kenya, William Ruto amewataka vijana nchini humo kutokubali kutumiwa na wanasiasa kwa maslahi yao ya kisiasa.
Aidha amesema kuwa serikali yake ina mpango wa vipengele vitano unaolenga kuwawezesha kiuchumi, kuongeza ajira na kuwasaidia kujitegemea.
Ruto amesema vijana hawafai kurubuniwa na baadhi ya viongozi wanaowatumia kama wanablogu wa kisiasa au makundi ya vijana wanaoshiriki vurugu za kisiasa badala ya kushughulikia changamoto zinazowakabili.
Ruto's call to empower youth
Akizungumza Ijumaa, Novemba 20, 2026, wakati akiendelea na ziara yake ya maendeleo katika eneo la Magharibi mwa Kenya, Rais huyo alisema serikali yake imeweka mikakati mbalimbali inayolenga kuhakikisha vijana wanapata fursa za ajira, elimu na mitaji ya kuanzisha biashara.
"Ninataka vijana wanisikilize. Msikubali wanasiasa kuwatumia kisiasa. Nina mpango mkubwa kwa ajili yenu. Msikubali kutumiwa kama wanablogu au wahuni wa kisiasa. Nina mpango wa vipengele vitano utakaohakikisha mnapata ajira na kuwezeshwa," alisema Ruto.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni mfumo mpya wa ufadhili wa masomo ya vyuo vikuu ambao Rais amesema unalenga kuhakikisha wanafunzi wanaendelea na masomo bila kukatizwa kutokana na changamoto za kifedha.
Aidha, serikali inalenga kuwasajili zaidi ya vijana 100,000 katika mpango wa mafunzo kazini (internship), ambapo kila mmoja anatarajiwa kulipwa Sh25,000 kabla ya kupata fursa za ajira za kudumu.
Kupitia mpango wa National Youth Opportunities Towards Advancement (NYOTA), Ruto alisema serikali tayari imetoa Sh50,000 kwa kila mmoja wa zaidi ya vijana 130,000 wenye ujuzi lakini wasio na ajira ili kuanzisha biashara zao.
Government initiatives for youth
Aliongeza kuwa serikali inalenga kupata vijana wengine 200,000 watakaonufaika na ufadhili huo wa kuanzisha miradi ya kibiashara.
Katika mpango mwingine, Rais alizungumzia mpango wa kuwawezesha vijana kupata zabuni za serikali kupitia mfumo wa Access to Government Opportunities (AGPO), akisema serikali inapanga kurahisisha upatikanaji wa zabuni hizo kwa kutumia simu za mkononi.
Vijana watasajiliwa, kupewa mafunzo ya wiki 10 na kusaidiwa kusajili kampuni zao bila malipo, huku serikali ikiahidi kuwalipa ndani ya siku 60 baada ya kuwasilisha bidhaa au huduma walizopatiwa zabuni.
Mpango wa tano unahusisha upanuzi wa ajira kupitia miradi ya nyumba za gharama nafuu, ujenzi wa masoko, vituo vya kidijitali vya ICT, pamoja na fursa za ajira nje ya nchi.
Job creation strategies discussed
Ruto alidai kuwa mpango wa ajira za nje ya nchi tayari umewanufaisha vijana 700,000.
Akizidi kuishambulia kambi ya upinzani, Rais aliwataka viongozi hao kueleza mikakati waliyonayo kwa vijana badala ya kuwatumia katika shughuli za kisiasa.
Ziara ya Ruto katika eneo la Magharibi inafanyika wakati wanasiasa wakizidisha juhudi za kujipanga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027, huku vijana wakiwa miongoni mwa makundi muhimu yanayowania ushawishi wa kisiasa.
Katika ziara hiyo, Rais ameandamana na viongozi kadhaa wa eneo hilo akiwemo Waziri Mkuu Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang'ula na Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya.









