Idadi ya watu wanaozikwa katika makaburi ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inaongezeka kwa kasi kubwa kuliko idadi rasmi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ebola, hali inayoashiria kuwa huenda ukubwa wa janga hilo umefichwa katika takwimu zinazotolewa na mamlaka za afya.

Uchunguzi uliofanywa na shirika la habari la Reuters kwa kutumia picha za satelaiti umebaini ongezeko kubwa la makaburi mapya katika maeneo ya Bunia na Mongbwalu, mkoani Ituri, ikilinganishwa na takwimu rasmi za vifo vilivyoripotiwa kutokana na mlipuko wa Ebola.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, idadi ya vifo vilivyozidi kiwango cha kawaida katika eneo la Bunia ilikuwa imefikia zaidi ya 1,000 kufikia mwanzoni mwa Novemba, ikiwa ni zaidi ya asilimia 50 ya vifo 707 vilivyokuwa vimeripotiwa rasmi kuhusishwa na Ebola katika kipindi hicho.

Uchambuzi huo pia unaonyesha kuwa pengo kati ya idadi ya mazishi na takwimu rasmi za vifo lilikuwa kubwa zaidi mwishoni mwa Juni, wakati idadi ya vifo vilivyobainika kupitia makaburi ilikuwa karibu mara saba ya takwimu rasmi za Ebola.

Hata hivyo, Reuters imeonya kuwa ongezeko hilo la vifo haliwezi kuhusishwa moja kwa moja na Ebola pekee, kwa kuwa linajumuisha pia watu ambao huenda walifariki kutokana na magonjwa mengine au kukosa huduma muhimu za afya wakati wa mlipuko huo.

Wafanyakazi wa makaburi waliozungumza na waandishi wa habari,wamesema idadi ya watu wanaozikwa iliongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya ugonjwa huo kuanza kusambaa mwezi Aprili, hali iliyozua maswali kuhusu usahihi wa taarifa zinazotolewa na mamlaka.

Baadhi ya sababu zinazochangia vifo kutorekodiwa ni pamoja na wagonjwa kuchelewa kugunduliwa, familia kukataa vipimo, hofu ya kwenda hospitalini, taarifa potofu kuhusu Ebola na udhaifu wa mifumo ya kufuatilia wagonjwa.

Uchunguzi huo umebaini kuwa zaidi ya asilimia 60 ya vifo vinavyohusishwa na Ebola vilitokea nje ya vituo vya afya, huku chini ya asilimia 15 ya maambukizi mapya yaliyothibitishwa yakitokana na watu waliokuwa tayari wanajulikana kuwa wamekutana na wagonjwa.

Hali hiyo inaonyesha kuwa maambukizi mengi yanaweza kuwa yalisambaa bila kufuatiliwa, huku mapambano dhidi ya ugonjwa huo yakiendelea kukabiliwa na changamoto za kiusalama na ukosefu wa rasilimali.