Mamlaka ya Ushuru nchini Kenya,(KRA) imezitaka kampuni na mashirika yote yanayohusika na ushuru wa Minimum Top-Up Tax (MTT) kujisajili na kutoa taarifa zao kabla ya Novemba 30, 2026, ili kuhakikisha zinatii matakwa mapya ya kodi nchini.

Kupitia notisi yake, KRA imeeleza kuwa kampuni zilizo chini ya mfumo huo zinapaswa kuitaarifu mamlaka hiyo kuhusu hali yao ya kuhusishwa na ushuru huo, huku zikipewa makataa ya mwisho ya Novemba 30 kuwasilisha taarifa zinazohitajika.

Kampuni hizo zinatakiwa kutoa jina la kundi la kampuni husika, nchi ambayo kampuni mama ya juu zaidi (Ultimate Parent Entity) imesajiliwa, pamoja na maelezo ya kampuni tanzu au taasisi nyingine zinazounda kundi hilo nchini Kenya.

Taarifa hizo zinapaswa pia kujumuisha nambari za utambulisho wa walipa kodi (PIN) za kila taasisi husika inayofanya shughuli zake nchini.

Aidha, KRA imeelekeza kampuni zinazohusika kuwasilisha marejesho ya ushuru wa Minimum Top-Up Tax na kulipa kiasi chochote cha kodi kitakachobainika kuwa kinadaiwa chini ya mfumo huo.

Mashirika hayo pia yanatakiwa kuzingatia Mkataba wa Kimataifa wa Mamlaka Husika kuhusu Ubadilishanaji wa Taarifa za GloBE (Multilateral Competent Authority Agreement on the Exchange of GloBE Information), unaowezesha nchi mbalimbali kubadilishana taarifa za kodi zinazohusiana na shughuli za makundi makubwa ya kampuni zinazofanya biashara katika mataifa tofauti.

Minimum Top-Up Tax ilianzishwa kupitia Kifungu cha 12G cha Sheria ya Ushuru wa Mapato (Income Tax Act), kabla ya kutekelezwa rasmi kupitia Kanuni za Ushuru wa Mapato (Minimum Top-Up Tax) za mwaka 2026.

Mfumo huo ni sehemu ya juhudi za kimataifa zinazolenga kuhakikisha makundi makubwa ya kampuni yanayofanya biashara katika mataifa mbalimbali yanalipa kiwango cha chini cha ushuru katika nchi ambako yanafanyia shughuli zao.

Hatua hiyo inalenga kuzuia kampuni kubwa za kimataifa kutumia tofauti za viwango vya kodi baina ya mataifa ili kupunguza kiwango cha ushuru kinachopaswa kulipwa.

KRA imewahimiza walipa kodi wote wanaohusika kuhakikisha wanatimiza masharti hayo ndani ya muda uliowekwa ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na kutowasilisha taarifa au marejesho ya kodi kwa wakati.