Mabadiliko ya umiliki wa nyumba na wosia wa mfanyabiashara Tob Cohen kabla ya kifo chake yameibuka katika kesi ya mauaji yake, huku wakili wake akieleza jinsi alivyositisha mpango wa kumshirikisha mkewe Sarah Cohen katika umiliki wa nyumba ya Kitisuru.

Wakili wake wa muda mrefu, Geoffrey Chege Kirundi, ameiambia mahakama kuwa Cohen alibadili msimamo kuhusu umiliki wa nyumba hiyo kabla ya kufanya mabadiliko makubwa katika wosia wake, akiondoa Sarah na binti yake kama wanufaika.

Kirundi, ambaye ni shahidi wa 26 wa upande wa mashtaka, amesema Cohen alimwagiza mwaka 2009 kuanzisha mchakato wa kuhamisha nyumba hiyo katika eneo la Kitisuru na kuifanya mali ya pamoja na mkewe.

Wakili huyo amesema nyumba hiyo ilikuwa imenunuliwa na Cohen kwa shilingi milioni 1.5 kabla ya kuifanyia maboresho na kuwa makazi yake.

Hata hivyo, Kirundi alimshauri Cohen dhidi ya hatua hiyo, akibainisha kuwa Sarah alikuwa tayari mnufaika pekee wa wosia wake uliokuwepo wakati huo.

Licha ya ushauri huo, Cohen alisisitiza kuwa mchakato wa uhamisho uendelee, hali iliyosababisha kuandaliwa kwa nyaraka muhimu za kisheria.

Lakini kabla ya shughuli hiyo kukamilishwa na kusajiliwa rasmi, Cohen alibadili uamuzi na kumwagiza wakili wake kusitisha mchakato huo.

Kirundi amesema Cohen alimweleza kuwa hakuwa tena na sababu ya kuendelea na uhamisho huo, hivyo nyumba hiyo ikaendelea kusajiliwa bila kuingizwa katika umiliki wa pamoja na Sarah.

Mahakama pia imeelezwa kuwa Cohen baadaye alibadilisha wosia wake, akimwagiza wakili huyo kuwaondoa Sarah na binti yake kama wanufaika na badala yake kuwateua mpwa wake wa kiume na wa kike.

Katika sehemu nyingine ya ushahidi wake, Kirundi alitilia shaka madai kwamba Cohen alikuwa amesafiri nje ya nchi baada ya kutoweka kwake.

Amesema Cohen alikuwa amemweleza awali kuwa hakuwa na mipango ya kusafiri hadi mwezi Oktoba, jambo lililoibua maswali kuhusu mazingira ya kutoweka kwake.

Ushahidi huo unaongeza uzito katika kesi ya mauaji ya Cohen, huku upande wa mashtaka ukiendelea kuwasilisha mashahidi na nyaraka za kuthibitisha mazingira yaliyopelekea kifo chake na matukio yaliyotangulia kutoweka kwake.