Ruto 'Apendekeza' Lydia Sitienei Kuwa Kamishna Wa Ulinzi Wa Data

Rais William Ruto amemteua wakili Lydia Sitienei kushika wadhifa wa Kamishna wa Ulinzi wa Data nchini, katika mabadiliko ya uongozi wa Ofisi ya Kamishna wa Ulinzi wa Data.

Sitienei anatarajiwa kuchukua nafasi ya Immaculate Kassait, ambaye amekuwa akihudumu katika wadhifa huo, iwapo uteuzi wake utaidhinishwa na Bunge la Kitaifa.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya Rais, Sitienei atahudumu kwa kipindi cha miaka sita iwapo atapata idhini ya wabunge, hatua itakayompa jukumu la kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni zinazohusu ulinzi wa taarifa binafsi nchini Kenya.

Ofisi ya Kamishna wa Ulinzi wa Data ni taasisi muhimu inayosimamia namna taasisi za serikali, kampuni binafsi na mashirika mengine zinavyokusanya, kuhifadhi, kutumia na kushughulikia taarifa za watu binafsi.

Taasisi hiyo pia ina jukumu la kuhakikisha kuwa haki za wananchi kuhusu faragha na matumizi ya taarifa zao binafsi zinalindwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Ulinzi wa Data ya mwaka 2019.

Iwapo uteuzi wa Sitienei utaidhinishwa, atakuwa na jukumu la kuendeleza juhudi za kuhakikisha kuwa mashirika yanayoshughulikia taarifa za wananchi yanafuata masharti ya kisheria, huku yakichukua hatua zinazofaa kuzuia matumizi mabaya ya data.

Aidha, ofisi hiyo ina jukumu la kupokea na kushughulikia malalamishi kutoka kwa watu wanaohisi kuwa taarifa zao binafsi zimetumiwa au kufichuliwa kinyume cha sheria.

Mchakato unaofuata ni Bunge la Kitaifa kupokea jina lake na kulifanyia uchunguzi wa kina kabla ya kufanya uamuzi kuhusu kuidhinisha au kukataa uteuzi huo.

Wabunge watakuwa na nafasi ya kutathmini taaluma yake, uzoefu wa kazi na uwezo wake wa kutekeleza majukumu yanayohusishwa na ofisi hiyo.

Uteuzi huo unajiri wakati ambapo matumizi ya teknolojia za kidijitali yanaendelea kupanuka nchini, huku masuala ya faragha, usalama wa taarifa na matumizi ya data yakiendelea kuwa muhimu katika sekta za umma na binafsi.

Kwenye teuzi za hivi juzi kati,asilimia kubwa imekuwa ni kwa vijana ambao sasa wameqminiwa na kupewa nafasi ya uongozi kwenye taifa lao.