Takriban watu 50,000 waliokimbia makazi yao nchini Ethiopia na kuvuka mpaka kuingia Kenya wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, maji safi na makazi bora katika eneo la Moyale, Kaunti ya Marsabit.
Familia hizo zimekuwa zikihangaika kupata mahitaji ya msingi tangu mwishoni mwa mwezi Oktoba, huku jamii zinazowahifadhi pia zikikabiliwa na changamoto ya rasilimali chache zinazohitajika kukidhi mahitaji ya wageni hao.
Kwa mujibu wa tathmini ya haraka iliyofanywa na mamlaka za Kenya kwa usaidizi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali, asilimia 71 ya kaya zilizofanyiwa utafiti hazina chakula cha kutosha.
Tathmini hiyo iliyohusisha kaya 758 imebaini kuwa asilimia 80 ya waliohojiwa wanataja chakula kuwa hitaji lao la dharura zaidi.
Hali ya upatikanaji wa maji safi na huduma za usafi pia imeibua wasiwasi, huku asilimia 44 ya kaya zikisema hazina maji ya kutosha ya kunywa.
Aidha, zaidi ya robo tatu ya familia hizo hazina vifaa au maeneo maalumu ya kunawia mikono.
Changamoto nyingine inayowakabili wahamiaji hao ni upatikanaji wa huduma za afya, huku zaidi ya nusu ya kaya zilizofanyiwa tathmini zikisema zinapata ugumu wa kupata matibabu kutokana na gharama kubwa na uhaba wa dawa.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, Mkuu wa Ujumbe wa IOM nchini Kenya, Nomagugu Ncube, amesema familia zilizokimbia makazi yao zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, maji na makazi, huku jamii zinazowapokea zikiwa tayari na rasilimali chache.
Jamii zinazowahifadhi nazo zakabiliwa na shinikizo
Wengi wa waliofika Moyale wamepata hifadhi kwa jamaa zao au familia za wenyeji, hali inayoongeza mahitaji ya chakula, maji na makazi katika jamii hizo.
Wengine wameelekea katika shule na maeneo ya muda yaliyotengwa kwa ajili ya kuwahifadhi, huku baadhi yao wakilazimika kulala nje bila makazi yanayofaa.
Tathmini hiyo imebaini kuwa asilimia 96 ya kaya zilizoshiriki zilikuwa zimetoroka kutoka maeneo ya Oromia na Somali nchini Ethiopia.
Jambo la kutia wasiwasi zaidi ni kuwa watu tisa kati ya kumi waliohojiwa walisema vijiji vyao vyote vilitoroka, ishara ya ukubwa wa hali ya kuhama kwa watu katika maeneo hayo.
IOM pia imeeleza kuwa zaidi ya nusu ya walioingia Kenya ni watoto, wakiwemo wengi walio chini ya umri wa miaka mitano, hali inayozua wasiwasi kuhusu afya na ustawi wao kutokana na kuzorota kwa mazingira wanamoishi.









