Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ameliomba Bunge la nchi hiyo kuondoa sheria inayoharamisha jaribio la mtu kujiua, akitaka manusura wa vitendo hivyo kuchukuliwa kama watu wanaohitaji msaada wa kiafya na kisaikolojia badala ya kukabiliwa na adhabu za kisheria.

Tinubu amewasilisha pendekezo la marekebisho ya sheria kwa Bunge la Seneti, hatua inayolenga kubadilisha mfumo wa sasa unaowaruhusu wahusika wanaojaribu kujiua kufunguliwa mashtaka na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo.

Katika barua iliyowasilishwa kwa Bunge, Rais huyo alisema marekebisho hayo yanalenga kuondoa uhalifu unaohusishwa na jaribio la kujiua na kuhakikisha watu wanaonusurika wanapata huduma za matibabu, ushauri nasaha na msaada wa kurejea katika maisha ya kawaida.

Pendekezo hilo limewasilishwa kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Afya ya Akili wa mwaka 2026 (National Mental Health Amendment Bill 2026), unaolenga kurekebisha Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2021.

Kwa sasa, jaribio la kujiua bado linachukuliwa kuwa kosa la jinai nchini Nigeria chini ya baadhi ya vifungu vya Sheria ya Makosa ya Jinai na Sheria ya Adhabu, ambapo mtu anayepatikana na hatia anaweza kufungwa hadi mwaka mmoja, kutozwa faini au kupewa adhabu zote mbili.

Hata hivyo, watetezi wa haki za watu wenye changamoto za afya ya akili wamekuwa wakipinga mfumo huo, wakisema kuwa kuwaadhibu manusura wa majaribio ya kujiua kunazidisha unyanyapaa na kuwazuia watu kutafuta msaada wa kitaalamu wanapokabiliwa na changamoto za kisaikolojia.

Kwa mujibu wa watetezi hao, hatua ya kujaribu kujiua inapaswa kuchukuliwa kama dharura ya kiafya inayohitaji uingiliaji kati wa wataalamu badala ya kuhusishwa na makosa ya jinai.

Muswada huo pia unapendekeza kuimarishwa kwa huduma za urekebishaji wa hali za manusura pamoja na kupanua upatikanaji wa huduma za afya ya akili nchini humo.

Kauli ya Tinubu imekuja wakati mjadala kuhusu kuondolewa kwa adhabu ya jaribio la kujiua ukiendelea katika Bunge la Nigeria, huku Seneta Godswill Akpabio, ambaye ni Spika wa Seneti, awali akikabiliwa na ukosoaji kutokana na kauli zake za kupinga hatua hiyo.

Hata hivyo, baada ya kupokea pendekezo la Rais, Akpabio alikaribisha marekebisho hayo na kusema watu wanaokabiliwa na changamoto za afya ya akili wanahitaji msaada badala ya kuadhibiwa.

Iwapo muswada huo utaidhinishwa, Nigeria itaungana na mataifa mengine ambayo yameondoa adhabu za jinai kwa watu wanaojaribu kujiua, na hivyo kuimarisha mtazamo unaotambua afya ya akili kama sehemu muhimu ya huduma za afya ya umma.