Hospitali ya Nairobi (The Nairobi Hospital) imefanya mabadiliko katika uongozi wake wa juu baada ya Afisa Mkuu Mtendaji (CEO), Felix Osano, kuondoka madarakani baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miezi 18.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa hospitali hiyo, Dkt. Barcley Onyambu, ametangaza kuondoka kwa Osano na kumteua Dkt. Magdalene Wambui Kamande kuwa kaimi Afisa Mkuu Mtendaji kuanzia Novemba 20, 2026.
Dkt. Kamande, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) pamoja na Huduma za Mabadiliko (Transformation Services), atashikilia nafasi hiyo kwa muda hadi bodi itakapoamua vinginevyo.
Katika taarifa ya ndani iliyotumwa kwa wafanyakazi wa hospitali hiyo pamoja na wanachama wa Chama cha Madaktari Wanaokubaliwa Kutoa Huduma Hospitalini (Admitting Staff Association), Onyambu alisema uteuzi huo umeanza kutekelezwa mara moja.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa Dkt. Kamande atatekeleza majukumu yote yanayohusiana na ofisi ya Afisa Mkuu Mtendaji kwa kuzingatia mfumo wa utawala wa hospitali, sera na taratibu zilizowekwa pamoja na mamlaka yatakayokabidhiwa kwake.
Bodi pia imewataka wafanyakazi na wanachama wa chama hicho kumpa ushirikiano, msaada na heshima ya kitaasisi ili aweze kutekeleza majukumu yake mapya kwa ufanisi.
Mabadiliko hayo ya uongozi yanajiri wakati ambapo hospitali hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za muda mrefu zinazohusiana na usimamizi na utawala wa taasisi, huku migogoro ya bodi ikisababisha mvutano mkubwa na hata kuhusisha mahakama pamoja na Bunge la Kenya.
Hospitali hiyo, inayomilikiwa na kuendeshwa na Kenya Hospital Association (KHA), imekuwa katika kipindi cha misukosuko ya kiutawala kutokana na kutokubaliana kuhusu uhalali wa baadhi ya viongozi, uteuzi wa wajumbe wa bodi na namna taasisi hiyo inavyosimamiwa.
Mnamo Agosti 2026, chama hicho kilifanya mabadiliko katika Bodi yake ya Usimamizi kufuatia Mkutano Mkuu wa Mwaka (AGM) uliofanyika Agosti 25, ambapo Onyambu alibakizwa katika nafasi ya mwenyekiti.
Bodi hiyo mpya ina wajumbe 11, huku wajumbe wanne wapya wakichaguliwa katika mkutano huo hatua iliyolenga kuimarisha muundo wa uongozi wa taasisi hiyo.
Osano alichukua nafasi ya uongozi baada ya aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji, James Nyamongo, kuondoka Desemba 2024 kufuatia kumalizika kwa mkataba wake.
Awali, Osano aliteuliwa kuwa kaimu CEO kabla ya kuthibitishwa rasmi katika nafasi hiyo Mei 2025.
Kabla ya kupandishwa katika nafasi ya juu ya uongozi, Osano alikuwa Mkurugenzi wa Ugavi (Supply Chain) katika hospitali hiyo na alikuwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 17 katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, uwekezaji na bidhaa za matumizi ya kila siku.
Kwa upande wake, Dkt. Kamande anakabidhiwa jukumu la kuongoza taasisi hiyo wakati ambapo inakabiliwa na matarajio ya kuimarisha usimamizi, kurejesha utulivu wa kiutawala na kuhakikisha utoaji wa huduma za afya unaendelea bila kuathiriwa na changamoto za ndani.
Hata hivyo, bodi haijatoa muda maalumu ambao Dkt. Kamande atahudumu katika nafasi hiyo ya kaimu.









