Zanzibar imepata fursa nyingine ya kujitangaza kimataifa kupitia sekta ya urembo na utalii baada ya kupokea mgeni maalumu, Miss World 2026 Joheirry Molla, aliyewasili visiwani humo Novemba 19, 2026, akiandamana na kundi la warembo wanaowakilisha mabara sita duniani.
Ujio wa mrembo huyo unatajwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii, utamaduni na vivutio vya kipekee, huku nchi ikiendelea kujiandaa kwa mashindano ya Miss World 2027 yanayotarajiwa kufanyika nchini.
Ziara hiyo inalenga kuonesha uzuri wa Tanzania kwa jukwaa la kimataifa, kwa kutumia ushawishi wa mashindano ya Miss World kufungua milango ya fursa mpya katika sekta ya utalii, biashara na uwekezaji.
Katika ziara yake Zanzibar, Molla anatarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria na vivutio vya utalii, pamoja na hoteli zinazoweza kuwa sehemu ya historia ya maandalizi ya mashindano hayo makubwa ya urembo duniani.
Zanzibar, inayotambulika kwa fukwe zake zenye mchanga mweupe, maji ya bahari ya kuvutia na urithi wa kihistoria, inatarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo yatakayosaidia kuonesha taswira halisi ya utajiri wa vivutio vya Tanzania kwa wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasili, Molla amesema amevutiwa na utamaduni wa Tanzania pamoja na mapokezi mazuri aliyoyapata, akieleza kuwa ana shauku ya kutembelea maeneo mbalimbali ya visiwa hivyo na kujionea mwenyewe uzuri wake.
Amesema ziara hiyo ni fursa ya kujifunza zaidi kuhusu maisha ya Watanzania, mila na desturi zao pamoja na vivutio vinavyofanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa maeneo yanayovutia watalii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Emmanuel Ishengoma, amesema Serikali inalenga kutumia maandalizi na uenyeji wa mashindano ya Miss World 2027 kama kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi.
Amesema mashindano hayo yanatoa nafasi ya kukuza utalii, kuimarisha sekta ya utamaduni na sanaa pamoja na kuitangaza Tanzania katika masoko mbalimbali ya kimataifa.
Aidha, amesema Serikali inatarajia kunufaika na mwonekano wa kimataifa unaoambatana na mashindano hayo, ikiwemo kuvutia wageni, wawekezaji na wadau wa sekta mbalimbali.
Mashindano ya Miss World ni miongoni mwa majukwaa makubwa ya urembo duniani, yanayokusanya washiriki kutoka mataifa mbalimbali na kutoa nafasi ya kuonesha vipaji, utamaduni na shughuli za kijamii.
Kwa Tanzania, maandalizi ya Miss World 2027 yanatarajiwa kuwa zaidi ya tukio la urembo, yakilenga kutumia jukwaa hilo kuonesha utambulisho wa taifa na kuongeza ushindani wake katika ramani ya utalii duniani.









