Serikali ya Somalia imechukua hatua kali za kidiplomasia dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), kwa kuitaka balozi wa nchi hiyo kuondoka nchini humo, huku ikitoa madai mazito kuhusu kile ilichokitaja kuwa ni kuingilia na kukiuka mamlaka ya taifa hilo.

Hatua hiyo imeashiria kuongezeka kwa mvutano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa na uhusiano katika masuala ya biashara, usalama na ushirikiano wa kikanda.

Waziri wa Habari wa Somalia, Abdifatah Kasim Mohamud, alitangaza uamuzi huo Alhamisi, Novemba 19, 2026, akisema serikali imeamua kumwondoa balozi huyo kama sehemu ya hatua za kulinda umoja, usalama na mipaka ya taifa hilo.

Aidha, Baraza la Mawaziri limeagiza Wizara ya Mambo ya Nje kumrejesha balozi wa Somalia aliyekuwa nchini UAE kwa mashauriano, hatua inayozidi kuonyesha kuzorota kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo.

Mohamud alitoa wito kwa raia wa Somalia kuungana katika kulinda nchi yao dhidi ya kile alichokitaja kuwa uvamizi wa wazi wa UAE, huku akionya kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya watu watakaoshirikiana na kile serikali inachodai kuwa ni juhudi za kukiuka mamlaka ya Somalia.

Hata hivyo, hakufafanua moja kwa moja vitendo maalumu vya UAE vilivyosababisha serikali kuchukua uamuzi huo.

Mvutano huo umeongezeka baada ya Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, kuishutumu UAE kwa kutoa msaada wa kisiasa na kiuchumi kwa baadhi ya serikali za maeneo yanayojitawala nchini humo ili kudhoofisha mamlaka ya serikali kuu iliyoko Mogadishu.

Rais huyo pia amedai kuwa UAE imekuwa ikiingia mikataba inayohusu bandari za Berbera, Bosaso na Kismayo moja kwa moja na tawala za maeneo hayo bila kuishirikisha serikali ya shirikisho.

Aidha, ameishutumu nchi hiyo kwa kusaidia kuanzishwa kwa vituo vya kijeshi na vikosi vya usalama vilivyo nje ya mfumo wa amri wa serikali kuu.

Kwa upande wake, UAE imekataa tuhuma hizo na kuishutumu serikali ya Somalia kwa kuchukua msimamo unaochochea uhasama na kudhoofisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE imesema inasikitishwa na kile ilichokitaja kuwa ni jitihada za Mogadishu kuingiza migogoro yake ya ndani katika uhusiano wa nchi hizo.

UAE pia ilifichua kuwa ilifunga ubalozi wake mjini Mogadishu na kuwaondoa wanadiplomasia wake Januari 2026, kufuatia kile ilichokitaja kuwa vitendo vya uhasama kutoka kwa serikali ya Somalia, ikiwemo kufutwa kwa mikataba ya ushirikiano.

Somalia ilikuwa imefuta mikataba yote na UAE iliyohusisha masuala ya bandari, ulinzi na usalama, ikidai kuwa ushirikiano huo ulikuwa unatishia mamlaka na umoja wa taifa hilo.

Mvutano huo unajiri wakati Somalia ikiendelea kukabiliwa na changamoto za kisiasa na kiusalama, huku serikali kuu ikikabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya tawala za kikanda pamoja na mapambano dhidi ya kundi la wanamgambo wa Alshabaab